SOKA

FIFA yaagiza ligi kuu ya Kenya msimu ujao uwe na vlabu 18

Nembo ya Shirikisho la kimataifa la Soka (FIFA) mbele ya shirikisho hilo mjini Zuric Oktoba 8, 2015.
Nembo ya Shirikisho la kimataifa la Soka (FIFA) mbele ya shirikisho hilo mjini Zuric Oktoba 8, 2015. AFP/AFP/Archives

Shirikisho la soka duniani FIFA, limeliagiza Shirikisho la soka nchini Kenya kuhakikisha kuwa vlabu 18 vinashiriki katika ligi kuu ya soka msimu ujao mwaka ujao. 

Matangazo ya kibiashara

Agizo hili linatarajiwa kumaliza mvutano kati ya kampuni inayosimamia ligi nchini humo KPL na Shirikisho la soka FKL  kuhusu ni vlabu vingapi vinavyostahili kushiriki ligi hiyo mwaka 2017.

KPL imekuwa ikitaka vlabu vinavyoshiriki ligi hiyo visalie 16 ikitoa sababu za kifedha kutoka kwa wafadhili huku viongozi wa soka nao wakitaka idadi hiyo kuongezeka kufikia 18 ili kuleta ushindani zaidi katika ligi hiyo.

Rais wa FKL Nick Mwendwa amesema amepata barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa FIFA Fatma Samoura, akimtaka kuhakikisha kuwa ligi kuu msimu ujao inakuwa na vlabu 18.

Mwendwa aliiandikia FIFA barua kuomba ushauri na ufafanuzi kuhusu kuongezwa kwa idadi ya vlabu vinavyocheza katika ligi hiyo.

KPL na FKL zilipelekana Mahakamani kujaribu kutafuta suluhu lakini Mahakama ikataka kuwe na masikilizano kati ya pande zote mbili.

Tume inayoshughulikia mizozo ya michezo nchini humo pia inasikiliza tofauti hizo wakati huu FIFA ikiwa imetoa uamuzi wake.