SOKA

Harambee Stars kuwakosa wachezaji watano wakati wa mchuano wa kirafiki na Msumbiji

Timu ya taifa ya soka ya Kenya Harambee Stars, itakosa huduma za wachezaji watano wakati itakapomenyana na Msumbiji katika mchuano wa Kimataifa wa kirafiki.

Timu ya taifa ya soka ya Kenya, Harambee Stars.
Timu ya taifa ya soka ya Kenya, Harambee Stars. youtube
Matangazo ya kibiashara

Mchuano huo utapigwa katika uwanja wa Kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi siku ya Jumamosi.

Kocha Stanley Okumbi amesema wachezaji watakaokosa mchuano huo ni pamoja na Ayub Timbe, Allan Wanga, Musa Mohammed, David Ochieng na Paul Were.

Timbe hatakuwepo kwa sababu anauguza jeraha huku Were na Ochieng wanaochezea Zesco United ya Zambia wakiomba kutofika Nairobi kwa sababu za mechi muhimu mwishoni mwa wiki hii.

Allan Wanga na Musa Mohammed nao wameomba udhuru kwa sababu wana shughuli za kibinafsi siku ya Jumamosi.

Mbali na mchuano huo, mataifa mbalimbali ya bara Afrika yanajiandaa kushuka dimbani mwishoni mwa wiki hii kumenyana katika hatua ya makundi kufuzu kucheza kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi.

Uganda ambayo ipo katika kundi la E pamoja na Misri, Ghana na Congo, siku ya Jumamosi itachuana na Congo katika uwanja wa Kimataifa wa Naambole jijini Kampala.

Kocha wa Cranes Micho Sredejovic amewaacha wachezaji watano kuelekea kwenye mchuano huu wakiwemo Sabban Juma na Yunus Santamu baada ya kupoteza mchuano wa Kimataifa dhidi ya Zambia kwa kufungwa bao 1-0 wiki hii jijini Kampala.

Rais Yoweri Museveni amekutana na wachezaji wa timu ya taifa na kula nao chakula cha mchana na kuwapongeza kwa kufuzu kwa fainali ya mataifa bingwa barani Afrika mwaka ujao nchini Gabon.