FORMULAR 1-HAMILTON

Bingwa wa dunia wa mashindano ya langalanga kujulikana katika mbio za mwisho za Abu Dhabi

Dereva Lewis Hamilton, akishangilia akiwa amesimama juu ya gari yake, katika mbio za Brazil Grand Prix, 13 Novemba 2016.
Dereva Lewis Hamilton, akishangilia akiwa amesimama juu ya gari yake, katika mbio za Brazil Grand Prix, 13 Novemba 2016. REUTERS/Paulo Whitaker

Mwendesha magari ya Langalanga ama "formular 1" Lewis Hamilton, amefanikiwa kushinda mbio za Brazil Grand Prix na kuweka hai zaidi matumaini yake ya kuwa bingwa wa dunia wa mbio hizo kwa mwaka huu, ambapo sasa mshindi atafahamika katika mbio za mwisho za Abu Dhabi.

Matangazo ya kibiashara

Licha ya mvua kubwa na ushindani mkali alioupata toka kwa dereva mwenzake wa Mercedez, Nico Rosberg, Hamilton bado alifanikiwa kumaliza kwenye nafasi ya kwanza kwa mtindo wa aina yake.

Mjerumani Nico Rosberg yeye alimaliza kwenye nafasi ya pili, na sasa kulazimika kushinda mbio za Novemba 27 mwaka huu ikiwa atataka kuchukua taji la ubingwa wa dunia wa mbio hizo, mbio za mwisho zikitajwa kama mbio za historia katika mashindano ya magari ya langalanga.

Dereva Nico Rosberg akisalimiana na dereva mwenzake wa kampuni ya Mercedes, Lewis Hamilton baada ya mbio za Mexico City.
Dereva Nico Rosberg akisalimiana na dereva mwenzake wa kampuni ya Mercedes, Lewis Hamilton baada ya mbio za Mexico City. Ulises Ruiz Basurto/Reuters

Wakati huu ni mbio moja tu ikiwa imesalia, Rosberg anaongoza kwa alama 12, huku Hamilton akiahidi kufanya kila linalowezekana kushinda taji la mwaka huu.

Dereva kinda Max Verstappen alionesha uwezo wa hali ya juu kwenye mbio za Brazil, na kumaliza kwenye nafasi ya tatu, baada ya awali kufanikiwa kutoka kwenye nafasi ya 16 hadi katika nafasi ya 3.

Huu ni ushindi wa kwanza wa Hamilton kwenye mbio za Brazil baada ya majaribio kama 10, ushindi ambao unamfanya amalize kwenye nafasi ya kwanza katika mbio tatu mfululizo akianzia na zile za Marekani na kisha Mexico.

Huu ni ushindi wa 9 wa Hamilton katika mwaka huu kati ya mbio 52 alizowahi kukimbiza gari, ambapo ikiwa atashinda mbio za Abu Dhabi, litakuwa ni taji lake la 4 la ubingwa wa dunia na kufikia rekodi ya muingereza Alain Prost.

Katika mbio zilizodumu kwa saa tatu na kushuhudia bendera nyekundu zikioneshwa katika raundi ya mwisho, na magari ya usalama kuingilia mbio hizo kwa zaidi ya mara 5, ajali pamoja na hisia, zilishuhudia dereva Sergio Perez akimaliza kwenye nafasi ya 4 akiwa na gari la kampuni ya Force India mbele ya dereva wa Ferrari, Sebastian Vettel.