OSCAR PISTORIUS

Oscar Pistorius ahamishiwa gereza la watu wenye mahitaji maalumu

Mwanariadha mwenye ulemavu, Oscar Pïstorius, akisindikizwa kutoka mahakani, mwaka 2013
Mwanariadha mwenye ulemavu, Oscar Pïstorius, akisindikizwa kutoka mahakani, mwaka 2013 REUTERS/Siphiwe Sibeko

Mwanariadha mwenye ulemavu Oscar Pistorius, ambaye anatumikia kifungo cha miaka 6 jela, amehamishwa kutoka kwenye gereza alikokuwa anazuiliwa na sasa atamalizia kifungo chake katika gereza la watu wenye mahitaji maalumu.

Matangazo ya kibiashara

Kitengo cha magereza nchini Afrika Kusini, kimesema kuwa mwanariadha huyo mwenye ulemavu wa miguu yote, amehamishwa kutoka gereza la Kgosi Mampuru II jijini Pretoria na kupelekwa gereza la Atteridgeville ambalo liko nje kidogo ya mji wa Pretoria.

"Uhamisho wake umezingatia mahitaji maalumu aliyonayo," amethibitisha msemaji wa kitengo cha magereza nchini humo, Singabakho Nxumalo.

"Gereza jipya linakidhi mahitaji ya watu wenye mahitaji maalumu, na hivi karibuni lilifanyiwa ukarabati ikiwa ni pamoja na kuongeza maeneo maalumu ya kuogea," alisema msemaji huyo.

Gereza hilo pia hutumika kuwaweka watu ambao wanatumikia kifungo cha chini ya miaka 6.

Mwezi Julai mwaka huu, Pistorius mwenye umri wa miaka 29, alihukumiwa kwenda jela miaka 6 na mahakama ya rufaa, baada ya adhabu ya awali ya kuua bila kukusudia kubadilishwa.

Awali alihukumiwa kifungo cha miaka 5 jela, na aliachiwa na kamati maalumu ya huduma za magereza inatopitia misamaha ya wafungwa.

Upande wa mashtaka bado unaendelea kupambana mahakamani ili kifungo hicho kiongezwe, wakidai kuwa adhabu aliyopewa ilikuwa ndogo ukilinganisha na kosa lenyewe.

Shujaa huyu wa zamani wa michezo ya Olimpiki kwa watu wenye ulemavu nchini Afrika Kusini, alimuua mchumba wake Reeva Steenkamp kwa kumpiga risasi, usiku wa kuamkia siku ya wapendanao mwaka 2013.