FIFA-ZAMBIA

Marekebisho ya katiba ya chama cha soka cha Zambia huenda yakakinzana na katiba ya nchi

Kikosi cha timu ya taifa ya Zambia.
Kikosi cha timu ya taifa ya Zambia. Reuters

Chama cha soka nchini Zambia (Faz) kimependekeza kufanyika mabadiliko ya katiba yake, mabadiliko ambayo ikiwa yatapitishwa, yatakinzana na sheria za nchi hiyo kuhusu watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

Matangazo ya kibiashara

Nchi ya Zambia imepiga marufuku mapenzi ya jinsia moja na mtu atakayepatikana akijihusisha atakabiliwa na kifungo cha miaka 15 jela.

Hata hivyo Faz inapitia katiba yake ya sasa na kutaka kuifanyia marekebisho, ili kuifanya iendane sambamba na sheria za shirikisho la kabumbu duniani Fifa.

Shirikisho la soka duniani Fifa linakataza vitendo vyovyote vya ubaguzi wa kijinsia, na yeyote anayeenda kinyume na sheria hiyo atafungiwa kabisa kujihusisha na masuala ya soka.

Mapendekezo ya rasimu ya katiba ya Faz yanasema "ubaguzi wa aina yoyote kwa nchi, mtu binafsi au kundi la watu na sehemu wanazotoka, rangi ya ngozi, ukabila, utaifa oa asili, jinsia, lugha, dini, mtazamo wa kisiasa, utajiri, uzaliwa, au ubaguzi wa kijinsia unakatazwa na adhabu yake ni kufungiwa ay kuondolewa kabisa."

Wakati mabadiliko haya yakienda sambamba na yale ya Fifa, ikiwa wajumbe wa Faz wataidhinisha kipengele hichi, shirikisho hilo huenda likaingia kwenye mgogoro wa kisheria na katiba ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa mashirika ya kutetea haki za binadamu, nchi ya Zambia ni miongoni mwa mataifa 35 ya Afrika ambayo kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja ni kosa kisheria.

Katibu mkuu wa Faz, Ponga Liwewe, alikanusha sintofahamu yoyote inayoweza kujitokeza na sheria za nchi ikiwa mabadiliko haya yataidhinishwa.

"Ni uamuzi wa wajumbe wa Faz kukubali au kukataa mabadiliko haya haya na baadae tuyaweke kwenye nyaraka ya mwisho ya chapisho la katiba yetu." alisema Liwewe.

Mjumbe wa Fifa, Primo Corvaro, mwezi Agosti mwaka huu aliendesha semina kuhusu marekebisho ya katiba ili yaendane na katiba ya Fifa.