FIFA

FIFA yafungua shauri la kinidhamu dhidi ya England na Scotland

Nahodha wa Uingereza Wayne Rooney akiwa amevaa kitambaa cheusi chenye kiua maarufu kama "Poppy"
Nahodha wa Uingereza Wayne Rooney akiwa amevaa kitambaa cheusi chenye kiua maarufu kama "Poppy" Reuters / Carl Recine Livepic

Shirikisho la kabumbu duniani FIFA, limefungua kesi ya kinidhamu dhidi ya timu ya taifa ya Uingereza na Scotland, baada ya wachezaji wa timu hizo kufaa vitambaa maalumu vilivyokuwa na kijiua chekundu "Poppy" ambacho hutumiwa kuwakumbuka raia wa Uingereza waliokufa kwenye vita.

Matangazo ya kibiashara

Hata hivyo FIFA haikusema ikiwa vitambaa hivyo vilivyovaliwa mkononi, vilikiuka sheria inayokataza mavazi yoyote yanayoashiria siasa, lakini kufunguliwa kwa kesi hii ni wazi kunaelekea kutolewa adhabu kwa timu hizo.

"Tunaweza kuthibitisha kuwa kesi ya kinidhamu imefunguliwa," amesema msemaji wa shirikisho la kabumbu FIFA wakati alipozungumza na shirika la habari la Ufaransa, AFP, wakati alipoulizwa kuhusiana na mchezo wa Novemba 11 uliozikutanisha timu hizo.

FIFA imesema kuwa, kwa sasa haiwezi kusema chochote cha ziada wala kubashiri matokeo ya shauri hilo.

Wachezaji wa timu zote mbili akiwemo kocha mkuu wa timu ya taifa ya Uingereza, Gareth Southgate, walivaa vitambaa vyeusi vilivyokuwa na kiua chekundu, kwenye mchezo wao uliopigwa katika dimba la Wimbley, na Uingereza kushinda kwa mabao 3-0.

Chama cha soka cha Uingereza kimesema kuwa kitakata rufaa kwa adhabu yoyote itakayotolewa dhidi yake, kwa kuwa inaamini kuwa ilikuwa ni haki yao na ilikuwa ni jambo la kimaadili.

Novemba 11, ni siku inayotambulika kama "Armistice Day", siku ambayo kitamaduni kwa nchi ya Uingereza, hutumiwa kuwakumbuka watu waliopoteza maisha wakati wa vita ya dunia.

Ireland ya Kaskazini pamoja na Wales walitaka kuvaa vitambaa vyenye kiua hicho, lakini baada ya kuwasiliana na FIFA na kupewa maelekezo, waliamua kuvaa vitambaa vyeusi pekee bila ya kupachika kiua chekundu.

Sheria za FIFA zinakataza timu kuvaa kitu chochote kinachoashiria mambo ya "kisiasa, dini, kauli mbiu ya mtu, tamko au picha".

Adhabu ya kosa hili ni pamoja na kunyang'anywa alama kwenye kundi lake la mechi za kufuzu kucheza kombe la dunia au kupigwa faini adhambo ambayo ndio ina uwezekano mkubwa kuchukuliwa dhidi ya timu hizo.

Hivi karibuni katibu mkuu wa FIFA, alisema kuwa nchi ya Uingereza na washirika wake, sio mataifa pekee duniani ambayo yalipoteza watu wao kwenye vita, na kwamba sheria hii ni lazima iwe inaheshimiwa na nchi zote wanachama zaidi ya 211 na isiwe ni jambo la kipekee kwa Uingereza na Scotland.