SOKA-KENYA

Tusker FC yakabidhiwa taji la ligi kuu ya soka nchini Kenya

Tusker FC wametawazwa rasmi mabingwa wa ligi kuu ya soka nchini Kenya baada ya kukamilika kwa msimu wa ligi kuu nchini humo msimu huu na kukabidhiwa kombe katika uwanja wa Nyayo  jijini Nairobi.

Mabingwa wapya wa soka nchini Kenya mwaka 2016
Mabingwa wapya wa soka nchini Kenya mwaka 2016 PHOTO | JEFF ANGOTE
Matangazo ya kibiashara

Mabingwa hawa wapya wenye makao yake katika mtaa wa Ruaraka jijini Nairobi, ulikuja wiki mbili zilizopita lakini, walikuwa wanasubiri mchuano wa mwisho siku ya Jumamosi dhidi ya mabingwa wa zamani Gor Mahia, ili kutawazwa rasmi.

Mabingwa hawa wapya walimaliza vizuri baada ya kupata ushindi katika mchuano wake wa mwisho, kwa kuifunga Gor Mahia bao 1-0 kupitia mshambuliaji Allan Wanga.

Baada ya mechi 30, Tusker FC imeshinda ligi kwa alama 61 huku Gor Mahia ikiwa ya pili kwa alama 54.

Ulinzi Stars imemaliza katika nafasi ya tatu kwa alama 46, Posta Rangers ya nne kwa alama 45 sawa na Chemelil Sugar ambayo imemaliza katika nafasi ya tano.

Tusker FC sasa imeshinda taji hili mara 11 mwaka 1972,1977,1978,1994,1996,1999,2000,2007,2011,2012 na 2016.

Gor Mahia bado inashikilia rekodi ya ubingwa nchini humo kwa kunyakua mataji 15 ikiwa ni pamoja na kushinda taji hilo mara tatu mfululizo mwaka 2013, 2014 na 2015.

Tusker FC sasa itawakilisha Kenya katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika mwaka ujao pamoja na taji la klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati CECAFA.

Katika hatua nyingine, Ushuru FC na Nairobi City Stars zimeshushwa daraja huku Sofapaka FC ikiponea kushushwa daraja baada ya kuifunga Thika United mabao 5-1.

Msimu ujao kwa mara ya kwanza unatarajiwa kuwa na timu 18.