KENYA-OLIMPIKI 2016

Uchunguzi: Maafisa wa Wizara ya Michezo walifuja fedha za kuwandaa wanamichezo wa Kenya

Boniface Mucheru bingwa wa Olimpiki mbio za Mita 400 kwa upande wa wanaume wakati Michezo ya Olimpiki nchini Brazil 2016
Boniface Mucheru bingwa wa Olimpiki mbio za Mita 400 kwa upande wa wanaume wakati Michezo ya Olimpiki nchini Brazil 2016 REUTERS/Alessandro Bianchi

Kiasi kikubwa cha fedha kichotengewa kugharamia kikosi cha Kenya kilichoshiriki katika Michezo ya Olimpiki mwaka huu nchini Brazil, zilifujwa.

Matangazo ya kibiashara

Hii imebainika baada ya kukamilika kwa uchunguzi uliofanywa katika Wizara ya Michezo nchini humo na kubaini kuwa, maafisa wa Wizara hiyo ndio waliohusika na kupotea kwa fedha hizo ambazo ni Mamilioni ya Shilingi za Kenya.

Ripoti ya uchunguzi ambayo bado haijawekwa wazi lakini Shirika la Habari la Uingereza Reuters imeiona, inasema fedha zilizokuwa zimetengewa kununua tiketi za wanamichezo mbalimbali, zilichukuliwa na maafisa wa Wizara ya Michezo.

Aidha, ripoti hiyo inaeleza kuwa Kamati ya Kenya ya Michezo ya Olimpiki (NOCK), ilitumia visivyo fedha zilizokuwa zimetolewa na kampuni ya Marekani ya Nike kununua jezi kwa wachezaji mbalimbali.

Suala lingine ambalo limebainika ni kuwa, wanariadha wamesema kampuni ya NOCK hupokea fedha kutoka kwa Nike kuwazawadia washindi wa medali katika Michezo ya Olimpiki.

Dola za Marekani 15,000 hutolewa kwa mshindi wa medali ya dhahabu, dola 7,500 kwa mshindi wa fedha na Dola 5,000 kwa mshindi wa shaba lakini wanariadha wamesema hawajawahi kupewa fedha hizo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Olimpiki nchini humo Kipchoge Keino amekanusha madai hayo na kusema wanariadha wamekuwa wakishughulika moja kwa moja na kampuni hiyo ya Nike.

Waziri wa Michezo nchini humo Hassan Wario aliyeagiza uchunguzi huo kufanywa amewasilisha ripoti hii kwa rais Uhuru Kenyatta.