CAF-SOKA

CAF yawafungia marefarii watatu kwa kufanya maamuzi mabaya mechi za kufuzu kombe la dunia

Shirikisho la soka barani Afrika CAF, limewafungia kwa muda wa miezi mitatu marefarii watatu kwa kuchezesha visivyo michuano miwili ya kufuzu kucheza fainali ya kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi.

Davies Omweno refarii wa Kenya, mmoja aliyefungiwa na CAF
Davies Omweno refarii wa Kenya, mmoja aliyefungiwa na CAF www.liberiaentertainment.com
Matangazo ya kibiashara

Marefarii hao ni pamoja na Mkenya Davies Omweno, Joseph Lamptey kutoka Ghana, Berhe O’Michael kutoka Eritrea na Theogene Ndagijimana kutoka Rwanda.

Hata hivyo, Ndagijimana yeye amepewa onyo kutokana na namna alivyofanya maamuzi kuhusu mchuano wa Libya na Tunisia.

Omweno ambaye amekuwa na rekodi nzuri mwaka huu anamaliza vibaya mwaka 2016 baada ya kulalamikiwa kuhusu mechi aliyokuwa refarii wa kati katika mchuano huo wa Libya na Tunisia akisaidiwa pia na Berhe O'Michael.

Watatu hao wamepatikana na kosa la kutokuwa makini wakati wa mchuano huo, na hivyo hatapewa tena nafasi ya kuwa uwanjani hadi mwaka 2017.

Kosa lingine ambalo Omweno ametuhumiwa kulifanya ni kutotoa adhabu kwa wachezaji katika mchuano huo lakini pia kusimama katika eneo lisilo sahihi kwa mujibu wa kanuni za CAF kuhusu uchezeshaji wa mchezo wa soka.

O'Michael naye amepatikana na kosa la kuinyima bao Libya kwa madai kuwa mchezaji wa timu hiyo alikuwa ameotea na hivyo kuifanya Tunisia kushinda kwa bao 1-0.

Joseph Lamptey ambaye alilalamikiwa sana wakati wa mchuano wa Afrika Kusini na Senegal uliomalizika kwa Afrika Kusini kushinda kwa mabao 2-1, amepewa adhabu hiyo kwa kuipa Afrika Kusini penalti na kuifanya kushinda mchuano huo.