SOKA-CAF

Nusu fainali ya michuano ya wanawake barani Afrika kurindima Jumanne

Nigeria ikichuana na Mali katika mchuano wa awali wa kundi B
Nigeria ikichuana na Mali katika mchuano wa awali wa kundi B cafoline

Hatua ya nusu fainali kutafuta ubingwa wa mchezo wa soka kwa upande wa wanawake barani Afrika, inachezwa siku ya Jumanne katika uwanja wa Ahmadou Ahidjo jijini Younde jijini Cameroon.

Matangazo ya kibiashara

Wenyeji Cameroon watakabiliana na Ghana huku mabingwa watetezi Nigeria wakichuana na Afrika Kusini.

Cameroon ilifuzu katika hatua hiyo baada ya kumaliza katika nafasi ya kwanza katika kundi A kwa alama 9 baada ya kuishinda Misri mabao 2-0, Afrika Kusini mabao 1-0 na baadaye Zimbabwe mabao 2-0.

Ghana nayo ikiwa katika kundi B, ilimaliza ya pili kwa alama saba baada ya kushinda michuano 2 kwenda sare moja na kutofungwa katika michuano mitatu iliyocheza.

Black-Queens walikuwa katika kundi moja pamoja na Nigeria, Kenya na Mali.

Mabingwa watetezi Super Falcons, ambao wameshinda mataji saba katika historia ya michuano hii, nayo walimaliza katika nafasi ya kwanza kwa alama 7 lakini wakiwa na mabao mengi.

Nigeria ilifanikiwa kupata mabao 11 huku Ghana ikawa na mabao 7.

Afrika Kusini ilianza kwa kupata sare ya kutofungana na Zimbabwe, ikafungwa na Cameroon bao 1-0 lakini ikafanikiwa kupata ushindi mkubwa wa mabao 5-0 dhidi ya Misri katika mchuano wake wa mwisho.

Mshambuliaji Asisat Oshoala anayecheza soka katika klabu ya Arsenal nchini Uingereza, anaongoza katika safu ya kuifungia Nigeria mabao 6 hadi sasa akifuatwa na Elizabeth Addo ambaye ameitikisia Ghana nyavu mara 3.

Fainali itachezwa siku ya Jumamosi.