SOKA

Brazil yaomboleza vifo vya wachezaji wa klabu ya Chapecoense FC

Mashabiki wa mchezo wa soka nchini Brazil wanaomboleza vifo vya wachezaji wa klabu ya Chapecoense, baada ya ndege ya abiria iliyokuwa inawasafirisha kuanguka ikikaribia mjini Medellin nchini Colombia.

Klabu ya  Chapecoense FC Novemba  23  2016
Klabu ya Chapecoense FC Novemba 23 2016 NELSON ALMEIDA / AFP
Matangazo ya kibiashara

Polisi wanasema kati ya abiria 81 waliokuwa ndani ya ndege hiyo, ni watano tu ndio walioponea lakini mtu mwingine wa sita ripoti zinasema ameokolewa.

Wachezaji hao walikuwa wanakwenda kushiriki katika michuano ya Copa Sudamericana, dhidi ya klabu ya Atletico Nacional yenye makao yake mjini Medellin.

Huu ulikuwa ni mchuano wa mzunguko wa kwanza kuwania taji hilo uliopangwa kuchezwa siku ya Jumatano lakini kwa sababu ya kutokea kwa ajali hii, mchuano huo umesitishwa.

Kabla ya kuanza kwa safari hiyo, Meneja wa klabu hiyo Cadu Gaucho alionekana katika mkanda video kwenye ukurasa wake wa facebook wa klabu hiyo akisema mchuano huo ulikuwa ni muhimu katika historia ya klabu hiyo.

Klabu hii iliundwa mwaka 1974, na imekuwa ikishiriki katika ligi kuu ya soka nchini Brazil tangu mwaka 2014 na msimu huu inaorodheshwa katika nafasi ya 9 mbele ya vlabu vingine maarufu kama Sao Paulo, Fluminense na Cruzeiro.

Ajali hii imekuja wiki moja baada ya kuwa klabu ya kwanza ya Brazil kufuzu katika fainali ya taji la Copa baada ya kuishinda San Lorenzo kutoka Argentina.