UINGEREZA-FA-SOUTHGATE

Southgate ateuliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Uingereza

Kocha wa timu ya taifa ya vijana ya Uingereza, chini ya umri wa miaka 21, Gareth Southgate.
Kocha wa timu ya taifa ya vijana ya Uingereza, chini ya umri wa miaka 21, Gareth Southgate. DR

Chama cha soka nchini Uingereza FA, kimemteua Gareth Southgate, kuwa kocha mkuu mpya wa kikosi cha timu ya taifa kwa mkataba wa miaka minne.  

Matangazo ya kibiashara

Southgate mwenye umri wa miaka 46 hivi sasa, alipandishwa ngazi na kuwa kocha wa muda akitokea kukinoa kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 21 mwezi Septemba mwaka huu baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa kocha mkuu Sam Allardyce.

Toka ameanza kukonoa kikosi cha wakubwa, Southgate ameiongoza timu yake kushinda mechi mbili na kutoka sare mechi mbili.

Southgate amesaini mkataba unaokadiriwa kuwa na thamani ya paundi za Uingereza milioni 2 kwa mwaka.

"Nimekuwa nafurahia sana kufanya kazi na wachezaji kwa majuma kadhaa yaliyopita hasa katika mechi nne na nadhani tuna nafasi kubwa na tuna vipaji," alisema Southgate.

Southgate, ameichezea Uingereza mara 57 na amekuwa maarufu sana baada ya kukosa penati muhimu wakati wa michuano ya kombe la Ulaya mwaka 1996 dhidi ya Ujarumani.

Anakuwa mchezaji wa kwanza wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza kukinoa kikosi hicho toka alipofanya hivyo kocha Kevin Keegan aliyekinoa kikosi hicho mwaka 2000.