SOKA

Rais wa Shirikisho la soka nchini Sudan Kusini ajiuzulu

Chabur Goc Alei  aliyekuwa rais wa Shirikisho la soka nchini Sudan Kusini
Chabur Goc Alei aliyekuwa rais wa Shirikisho la soka nchini Sudan Kusini FIFA

Chabur Goc Alei amejiuzulu kuwa rais wa Shirikisho la soka nchini Sudan Kusini, siku chache baada ya Bodi kuu ya Shirikisho hilo kumsimamisha kazi.

Matangazo ya kibiashara

Bodi hiyo ilifikia uamuzi huo baada ya kumtuhumu rais huyo kwa kutumia vibaya fedha za Shirikisho hilo zilizotengwa kuendeleza mchezo wa soka nchini humo.

Nafasi ya Chabur sasa itachukuliwa na naibu wake Andrea Abdella, hadi mwezi Machi mwaka ujao wakati uchaguzi mwingine wa kumpata rais mpya utakapofanyika.

Chabur ameahidi kukabidhi madaraka kwa amani wakati atakaporejea nchini humo hivi karibuni.

“Nawashukuru sana rafiki zangu kwa uamuzi mliochukua dhidi yangu, licha ya sisi wote kuanza safari hii. Nilifikiri tutamaliza pamoja safari hii tuliyoanza pamoja lakini mmeamua nipigwe risasi na rafiki zangu wala sio maadui zangu,” aliandika katika ukurasa wake wa facebook.

Bodi ya Shirikisho hilo linadai kuwa Chabur, alipeleka Dola za Marekani 400,000 katika kaunti yake ya kibinafsi mwaka 2015 lakini pia kuamua kukopa Dola 12,000 kama mtu binafsi kwa niaba ya Shirikisho hilo.