FIFA-SOKA

Baraza la FIFA kupigia kura pendekezo la kuongeza mataifa yatakayofuzu kombe la dunia

Rais wa Shirikisho la soka duniani FIFA Gianni Infantino
Rais wa Shirikisho la soka duniani FIFA Gianni Infantino FIFA.COM

Baraza Kuu la Shirikisho la soka duniani FIFA, linakutana jijini Zurich nchini Uswizi, kupigia kura mapendekezo ya kuongeza idadi ya mataifa yatakayoshiriki katika michuano ya kombe la dunia kuanzia mwaka 2026.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa FIFA Gianni Infantino, wakati wa kampeni mwaka uliopita akiomba kuchaguliwa katika nafasi hiyo, aliahidi kuongeza idadi ya mataifa yatakayoshiriki katika michuano hiyo kutoka 32 hadi 48.

Ikiwa Baraza hilo litakubali pendekezo la Infantino, itakuwa mara ya kwanza kwa mataifa yanayoshiriki katika michuano hiyo kuongezeka tangu mwaka 1998.

Baraza hilo la wajumbe 37, lina nafasi ya kuchagua pendekezo la kuwa na mataifa 48 yatakayojumuishwa katika makundi 16, kila kundi likiwa na timu tatu.

Mbali na hilo, wajumbe hao watakuwa na nafasi pia ya kuamua mataifa hayo 48 yatashiriki katika michuano ya mwondoano na kusalia na mataifa 32 yatakayopangwa katika hatua makundi.

Ikiwa mapendekezo hayo yatapitishwa, hayatatumika katika michuano ya mwaka 2018 nchini Urusi na 2022 nchini Qatar.

Infatino amesema ongezeko hilo, litasaidia kuongezeka kwa mataifa yanayoshiriki katika kombe la dunia kutoka barani Afrika na barani Asia.

Hata hivyo, kuna baadhi ya wadau wa soka wanaopinga pendekezo hili kwa madai kuwa kuwepo kwa mataifa mengi yatafifisha ushindani katika michuano hii.