FIFA-SOKA

FIFA yaridhia mataifa 48 kucheza kombe la dunia kuanzia mwaka 2026

Shirikisho la soka duniani FIFA, kwa kauli moja, limekubali kuongeza idadi ya mataifa yatakayoshiriki katika michuano ya kombe la dunia kutoka mataifa 32 hadi 48 kuanzia mwaka 2026.

Rais wa Shirikisho la soka duniania FIFA, Gianni Infantino
Rais wa Shirikisho la soka duniania FIFA, Gianni Infantino REUTERS/Arnd Wiegmann
Matangazo ya kibiashara

Wajumbe 37 waliokutana katika makao makuu ya FIFA mjini Zurich, wameamua kuwa mataifa 48 yatakayokuwa yamefuzu, yatapangwa katika makundi 16 huku kila kundi likiwa na timu tatu zitakazoshiriki katika hatua ya mwondoano.

Baada ya michuano hiyo ya mwondoano, mataifa 32 yatakayokuwa yamepatikana, yatapangwa katika makundi manane, kila kundi likiwa na timu nne.

Mabadiliko haya yanamaanisha kuwa, michuano itakayochezwa katika kombe la dunia, itaongezeka kutoka 64 hadi 80.

Siku za michuano hiyo ya kombe la dunia itachezwa ndani ya siku 32, uamuzi ambao umelifurahisha Shirikisho la soka barani Ulaya UEFA, ambalo lilikuwa na hofu ya ratiba zake kuathirika.

Pendekezo hili, liliwasilishwa na rais wa FIFA Gianni Infantino mwaka 2016, wakati wa kampeni ya kuchaguliwa katika nyadhifa hiyo kwa kile alichokisema kuwa hatua hiyo itafanya kombe la dunia kujumuisha mataifa mengi.

Mara ya mwisho kwa FIFA kuongeza idadi ya mataifa yanayoshiriki katika fainali hii ilikuwa ni mwaka 1998.

Bara la Afrika na Asia yanaelezwa kuwa ndio yatanufaika pakubwa na ongezeko hili.

Afrika ambayo huwa ina wawakilishi watano katika michuano hii, idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka na kufikia saba.

Angalia Historia ya mabadiliko ya mataifa yanayoshiriki katika kombe la dunia:-

 • 1930 nchini Uruguay Mataifa-13
 • 1934 nchini Italia Mataifa- 16
 • 1950 nchini Brazili mataifa -13
 • 1954 nchini Uswizi mataifa-16
 • 1958 nchini Sweden mataifa-16
 • 1974 nchini West Germany mataifa-16
 • 1982 nchini Uhispania mataifa-24
 • 1986 nchini Mexico-24
 • 1998 nchini Ufaransa mataifa-32
 • 2002-2022- Mataifa 32
 • 2026-Mataifa 48