SOKA-AFCON 2017

Hatimaye michuano ya AFCON 2017 kuanza nchini Gabon

Shabiki wa Gabon akisubiri mchuano wa leo kati ya nchi yao na Guinea-Bissau
Shabiki wa Gabon akisubiri mchuano wa leo kati ya nchi yao na Guinea-Bissau AFP PHOTO/Franck Fife

Makala ya 31 ya michuano ya soka kuwania ubingwa wa bara Afrika yanafunguliwa Jumamosi hii jijini Libreville nchini Gabon.

Matangazo ya kibiashara

Mechi ya ufunguzi ni kati ya wenyeji Gabon na Guinea-Bissau kuanzia saa moja usiku saa za Afrika Mashariki katika uwanja wa Kimataifa wa Stade de l'Amitie jijini Libreville.

Gabon nayo itakuwa nyumbani kutafuta ushindi wake wa kwanza, wakiongozwa na nahodha na mchezaji anayetegemewa sana Pierre-Emerick Aubemayang.

Guinea-Bissau nayo iliyowashangaza wengi kwa kufuzu katika michuano hii kwa mara ya kwanza, inasubiriwa kuona namna itakavyopambana uwanjani katika mchuano huu wa ufunguzi.

Sikiliza maoni ya wasikilizaji

Wachambuzi wa soka wanasema, mchuano wa leo hautakuwa na shinikizo kwa Guinea-Bissau ikilinganishwa na Gabon ambao watakuwa mbele ya mashabiki wa nyumbani na hivyo watahitaji kushindi.

Mchuano wa pili utakuwa ni kati ya Cameroon na Burkina Faso, kuanzia saa nne usiku saa za Afrika Mashariki.

Cameroon inayofahamika kama The Indomitable Lions , inajivunia wachezaji kama Guy N’dy Assembé, André Onana, Joël Matip, Allan Nyom, Maxime Poundjé, Ibrahim Amadou, André-Frank Zambo Anguissa na Eric Maxime Choupo-Moting ambao wamesifiwa kuwa bora na shupavu kipindi hiki.

Burkina Faso ambayo mwaka 2013, ilifika katika hatua ya fainali na kwa bahati mbaya kufungwa na Nigeria, nayo inajivunia wachezaji kama Jonathan Pitroïpa, Aristide Bancé na Charles Kaboré wanaotarajiwa kuwaongoza wenzao kupata ushindi.

Mzozo wa kisisa
Michuano hii inaanza nchini Gabon wakati huu kukiendelea kushuhudiwa wasiwasi wa kisiasa kati ya rais Ali Bongo na mpinzani wake Jean Ping.

Ping anadai kuwa, rais Bongo aliiba kura mwaka uliopita, na wafuasi wake wamepanga kuandamana wakati wa ufunguzi wa michuano hii kuonesha gadhabu zao.

Upinzani, umewataka wafuasi wake kususia michuano hii kama ishara ya kumpinga rais Bongo.

Michuano hii imekuja wakati huu nchi hiyo ikiendelea kupitia wakati mgumu wa kiuchumi, suala ambalo limeilazimu kamati andalizi kupunguza bei ya tiketi ambazo sasa zinauzwa kwa kati ya Dola 0.81 na Dola 65.

Mataifa 16 yanashiriki katika michuano hii.

Mataifa hayo ni pamoja na:-

  • Kundi A- Gabon (Wenyeji), Burkina Faso, Cameroon, Guinea-Bissau
  • Kundi B-Algeria, Tunisia, Senegal, Zimbabwe
  • Kundi C-Ivory Coast,DR Congo,Morocco, Togo
  • Kundi D-Ghana, Mali, Misri, Uganda

Uchambuzi wa kina wa mataifa yanayoshiriki katika michuano hii: Soma zaidi

Michuano hii itamalizika mwezi Februari tarehe 5.

Mabingwa watetezi ni Ivory Coast.