AFCON 2017-GABON

Afcon 2017: Senegal yaanza vema, Algeria na Zimbabwe zagawana alama

Wachezaji wa timu ya taifa ya Senegal, wakishangilia moja ya bao baada wa kuifunga Tunisia.
Wachezaji wa timu ya taifa ya Senegal, wakishangilia moja ya bao baada wa kuifunga Tunisia. ©Pierre René-Worms

Michuano ya kombe la mataifa ya Afrika imeendelea kutimua vumbi nchini Gabon, huku mwishoni mwa juma michezo ya kundi A na B ikipigwa.

Matangazo ya kibiashara

Jumapili ya Januari 15, timu ya taifa ya Zimbabwe ilikuwa na kibarua dhidi ya mbweha wa jwangwani, timu ya taifa ya Algeria, katika mchezo ulioshuhudia kabumbu la aina yake kutoka kwa timu zote mbili.

Walikuwa ni Algeria ambao ndio waliokuwa wa kwanza kuandika bao katika dakika ya 12 ya mchezo kupitia kwa winga wake Riyad Mahrez, aliyewazidi ujanja mabeki wa Zimbabwe na kuukwamisha mpira nyavuni.

Hata hivyo dakika tano baadae Zimbabwe walifanikiwa kusawazisha bao hilo kupitia kwa Kudakwashe Mahachi, aliyepiga shuti lililotinga moja kwa moja nyavuni, dakika chache baadae, bao la Nyasha Mushekwi kupitia njia ya penati, liliwafanya Zimbabwe kuongoza kabla ya dakika ya 82, Ruyad Mahrez kuisawazishia timu yake.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Zimbabwe wakishangilia moja ya goli walilofunga dhidi ya Zimbabwe.
Wachezaji wa timu ya taifa ya Zimbabwe wakishangilia moja ya goli walilofunga dhidi ya Zimbabwe. ©Pierre René-Worms

Mchezo huu ulishuhudia timu hizi zikitoshana nguvu ya sare ya mabao 2-2.

Kikosi cha Georges Leekens itabidi kijilaumu chenyewe kwa kushindw akutumia vema nafasi ilizozipata, sawa na kwa kocha wa Zimbabwe Calisto Pasuwa ambaye wachezaji wake hawakuwa makini kwenye lango.

Katika mchezo mwingine, Simba wa Teranga, timu ya taifa ya Senegal yenyewe ilikuwa na kibarua dhidi ya timu ya taifa ya Tunisia, katika mchezo mwingine ambao hata hivyo ulitawaliwa pakubwa na Senegal.

Tunisia alimanusura wawe wa kwanza kuandika bao kupitia kwa mshambuliaji wake Ahmed Akaichi, lakini hata hivyo kichwa chake hakikulenga goli.

Dakika chache baadae, beki wa Tunisia, alimuangusha kwenye eneo la hatari kiungo Cheikhou Kouyate, na mshambuliaji Sadio Mane anayekipiga na Liverpool ya Uingereza alichukua jukumu la kupiga mkwaju wa penati na kuiandikia timu yake bao la kuongoza.

Dakika ya 30, mchezaji wa Senegal, Kara Mbodji aliiandikia timu yake bao la pili, akitumia mpira wa krosi, na kupiga kichwa kilichotinga moja kwa moja kwenye nyavy za Tunisia.

Kwa matokeo haya, Senegal wanaongoza kwenye kundi B, ikiwa na alama tatu, ikifuatiwa na Algeria na Zimbabwe zenye alama moja moja.

Michuano hii inatarajiwa kuendelea tena Jumatatu ya tarehe 16, ambapo timu ya taifa ya Cote d'Ivoire itakuwa na kibarua dhidi ya timu ya taifa ya Togo katika mchezo utakaopigwa kwenye dimba la Oyem, majira ya saa moja kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Mchezo mwingine utawakutanisha wawakilishi kutoka ukanda wa nchi za maziwa makuu timu ya taifa ya DRC, ambayo yenyewe itawakaribisha timu ya taifa ya Morocco, katika mchezo ambao utapigwa kwenye dimba la Franceville majira ya saa nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki.