AFCON 2017-GABON

Afcon 2017: Togo yaibana Ivory Coast, DRC yafanya kweli licha ya kucheza pungufu

Mchezaji wa Togo, Emmanuel Adebayor akiruka juu mbele ya wachezaji wa Côte d'Ivoire, 16JAN2017
Mchezaji wa Togo, Emmanuel Adebayor akiruka juu mbele ya wachezaji wa Côte d'Ivoire, 16JAN2017 Pierre René-Worms

Mechi za kundi C katika michuano ya kombe la mataifa ya Afrika inayoendelea kutimua vumbi nchini Gabon, zimepigwa Jumatatu ya wiki hii, na kushuhudia mabingwa watetezi Ivory Coast wakilazimishwa sare ya bila kufungana na Togo.

Matangazo ya kibiashara

Kwenye mchezo huo ambao wengi waliipa nafasi timu ya taifa ya Ivory Coast kuibuka na ushindi, lakini mambo hayakuwa hivyo kwani Togo wanaonolewa na kocha Claude Le Roy, walitoa upinzani mkubwa kwa Ivory Coast na kulazimisha sare ya bila kufungana.

Ivory Coast waliokuwa wanaongozwa na nahodha, Die Gnozaroua Serey, walishindwa kufua dafu mbele ya Togo waliokuwa wakiongozwa na nahodha ambaye hana timu hivi sasa kwa zaidi ya miezi sita, Emmanuel Adebayor.

Licha ya kuwa na kikosi kilichosheheni wachezaji wanaocheza soka la kulipwa kwenye nchi nyingi za Ulaya, Ivory Coast hawakuonesha kiwango ambacho wengi walitarajia labda wangekionesha kama mabingwa watetezi.

Kiungo Wilfred Zaha ambaye ilikuwa ni mechi yake ya kwanza ya kimashindano na timu ya taifa ya Ivory Coast toka alipoamua kuikacha timu ya taifa ya Uingereza, alishindwa kuonesha makeke yoyote licha ya kutengeneza nafasi kadhaa.

Mechi nyingine ya kundi C iliwakutanisha wawakilishi kutoka ukanda wa nch za maziwa makuu, timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, ambayo ilikuwa ikipepetana na timu ya taifa ya Morocco inayonolewa na kocha Harve Renard.

Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Morocco, Hervé Renard.
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Morocco, Hervé Renard. AFP/Fethi Belaid

Morocco licha ya kuanza kipindi cha kwanza kwa kuonesha soka la aina yake, washambuliaji wake hawakuwa makini mbele ya lango la DRC, kwani licha ya kutengeneza nafasi kadhaa, walishindwa kuzitumia vema.

Pengine kocha wa Morocco, Harve Renard, huenda akajutia uamuzi wake wa kumuweka benchi mshambuliaji wake wa kimataifa, YOUSSEF EL ARABI, ambaye aliingia kipindi cha pili akitokea benchi na kuonekana wazi kuisumbua ngome ya DRC, iliyokuwa ikiongozwa na nahodha, GABRIEL ZAKUANI.

Licha ya mashambulizi yote haya na kumiliki mpira kwa kiwango kikubwa, Morocco walijikuta wakipoteza mchezo huo, chini ya kikosi cha kocha mzawa Florent Ibenge, ambaye bao la mchezaji, HARVE KAGE, lilitosha kuzamisha jahazi la Morocco.

DRC wanahitaji pongezi kwani licha ya kucheza kumi uwanjani baada ya mchezaji wao, Joyce Lomalisa Mutambala, kutolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kuzawadiwa kadi mbili za njano kwenye mchezo huo.

Hii leo mechi za kundi D zitapigwa, ambapo wawakilishi pekee kutoka ukanda wa nchi za Afrika Mashariki, timu ya taifa ya Uganda "Uganda Cranes" itashuka uwanjani majira ya saa kumi na mbili kamili jioni kupepetana na timu ya taifa ya Ghana "Black Stars", mchezo huu utapigwa kwenye dimba la "Stade de Port Gentil".

Mechi nyingine ya kundi D, itawakutanisha timu ya taifa ya Mali ambayo itashuka dimbani kupepetana na waliowahi kuwa mabingwa pia wa michuano hii, timu ya taifa ya Misri, mchezo utakaopigwa majira ya saa nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki, huku kipute kikipigwa kwenye uwanja huo huo.