SOKA-AFCON 2017

Algeria yatupwa nje michuano ya AFCON, Zimbabwe yashindwa vibaya

Algeria ikimenyana na Zimbabwe katika mchuano muhimu wa AFCON Januari 23 2017
Algeria ikimenyana na Zimbabwe katika mchuano muhimu wa AFCON Januari 23 2017 Pierre René-Worms/RFI

Timu ya taifa ya soka ya Algeria imeondolewa katika michuano ya kusaka taji la bara Afrika AFCON, kwa kutopata ushindi wowote katika hatua ya makundi.

Matangazo ya kibiashara

Vijana wa Algeria wanarejea jijini Algers baada ya  kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Senegal katika mchuano wake wa kundi B mjini Franceville nchini Gabon siku ya Jumatatu usiku.

Mchuano wa kwanza, Algeria ilitoka sare ya mabao 2-2 na Zimbabwe lakini ikafungwa na Tunisia mabao 2-1.

Mbali na Algeria, Zimbabwe pia imeyaanga mashindano haya baada ya kumaliza wa mwisho katika kundi hilo kwa alama 1.

Mchuano wake wa mwisho, Brave Warriors walishindwa vibaya, baada ya kufungwa na Tunisia mabao 4-2.

Tunisia ilipata mabao yake yote katika kipindi cha kwanza cha mchuano huo katika dakika ya 9 ,22, 36 na 45 huku Zimbabwe ikijipatia mabao yake katika dakika ya 42 na 58.

Kikosi
Zimbabwe: Mukuruva, Nhamoinesu, Phiri, Zvirekwi, Muroiwa, Bhasera, Mushekwi, Katsande, Musona, Nakamba, Billiat.

Tunisia: Jeridi, Ben Youssef, Abdennour, Msakni, Khazri, Khenissi, Maaloul, Sassi, Ben Amor, Naguez, Naim.

Siku ya Jumanne, mechi za kutamatisha kundi C zitachezwa katika uwanja wa Oyem.

Morocco itamenyana na Ivory Coast huku Togo ikimenyana na DR Congo, mechi zitazochezwa kuanzia saa nne kamili saa za Afrika Mashariki.

Mabingwa watetezi Ivory Coast wanahitaji ushindi katika mchuano wa leo ili kujipa matumaini ya kusonga mbele kwa sababu ina alama 2, huku wapinzani wao wa leo wakiwa na alama tatu.

DR Congo ina alama nne, huku Togo ikiwa ya mwisho kwa alama moja.

Ratiba ya robo fainali
Januari 28 2017

  • Burkina Faso vs Tunisia-Mechi itacheza katika uwanja wa Libreville.
  • Senegal vs Cameroon-Mechi itachezwa katika uwanja wa Franceville.

Januari 29 2017

  • Mshindi wa kundi C vs Mshindi wa pili wa kundi D.
  • Mshindi wa kundi D vs Mshindi wa pili wa kundi C.