AFCON 2017

Kocha wa Algeria Georges Leekens abwaga manyanga

Kocha wa Algeria Georges Leekens
Kocha wa Algeria Georges Leekens KHALED DESOUKI / AFP

Kocha wa timu ya taifa ya Algeria Georges Leekens amejiuzulu siku moja baada ya timu yake kuondolewa katika michuano ya mataifa bingwa barani Afrika nchini Gabon.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hii inakuja baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Senegal katika mchuano wake hapo wa mwisho wa hatua ya makundi.

Desert Foxes kama wanavyofahamika, walikwenda katika mchuano huo kama mojawapo ya timu inayopewa nafasi kubwa kushinda taji hili.

Mbali na sare ya Jumatatu, ilitoka sare ya mabao 2-2 na Zimbabwe huku wakifungwa na Tunisia mabao 2-1.

Kocha Leekens mwenye umri wa miaka 67 kutoka Ubegiji alianza kuifunza Algeria mwezi Oktoba mwaka uliopita, miezi mitatu kabla ya michuano hii kuanza.

Mwaka 2003 aliwahi pia kuifunza Algeria lakini kati ya mwaka 2014-2015 alikuwa kocha wa timu ya taifa ya Tunisia.