AFCON 2017

Mabingwa watetezi Ivory Coast waondoka Gabon mikono mitupu

Mshambuliaji wa Ivory Coast  Wilfried wakati wa mchuano dhidi ya Morocco
Mshambuliaji wa Ivory Coast Wilfried wakati wa mchuano dhidi ya Morocco Pierre René-Worms / RFI

Mabingwa watetezi wa taji la soka barani Afrika, Cote Dvoire, wameondolewa katika makala ya 31 ya michuano ya AFCON inayoendelea nchini Gabon.

Matangazo ya kibiashara

Haya ni matokeo mabaya kwa wafalme hawa soka barani Afrika, baada ya kuondolewa katika hatua ya makundi siku ya Jumanne, bila ya kupata ushindi wowote katika kundi C.

Matumaini ya Ivory Coast yalididimia baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Morocco katika mchuano muhimu wa mwisho katika kundi hilo na kupoteza alama tatu muhimu.

Katika mechi tatu ilizocheza, ilitoka sare ya kutofungana na Togo, lakini baadaye ikatoka sare nyingine ya mabao 2-2 na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Matokeo haya yameleta huzuni kubwa kwa mashabiki wa soka nchini Ivory Coast ambao walikuwa na matumaini makubwa kuwa kikosi cha kingerudi jijini Abidjan na kombe hili.

Aidha, ni pigo kubwa kwa serikali iliyotumia fedha nyingi, Dola Milioni 6 kukiandaa kikosi hiki na kuwalipa marupurupu wachezaji wa timu ya taifa soka.

Morocco wanaofunzwa na kocha wa zamani wa Ivory Coast Mfaransa Herve Renard walikwenda katika mchuano huu wakiwa na matumaini na nidhamu ya hali ya juu kutafuta ushindi dhidi ya wapinzani wao.

Bao la Rachid Alioui katika dakika 64 lilitosha kuwafurusha virago Morocco ambao wamefuzu katika hatua ya robo fainali.

Morocco sasa itacheza na mshindi wa kundi D, kati ya Ghana na Misri.