SOKA-UEFA

Matumaini ya Arsenal kusonga mbele michuano ya UEFA yadidimia

Matumaini ya klabu ya soka ya Arsenal kutoka Uingereza kufuzu katika hatua ya robo fainali kuwania taji la michuano ya klabu bingwa barani Ulaya UEFA  msimu huu, yamekatizwa ghafla baada ya kufungwa na Bayern Munich ya Ujerumani mabao 5-1.

Mchuano wa mzunguko wa kwanza wa mwondoano kati ya Bayern Munich na Arsenal Februari 15 2017
Mchuano wa mzunguko wa kwanza wa mwondoano kati ya Bayern Munich na Arsenal Februari 15 2017 REUTERS
Matangazo ya kibiashara

Ni wazi kuwa Arsenal haitakuwa na kazi rahisi nyumbani mwezi ujao itakapoikaribisha Bayern Munich jijini London, baada ya kushindwa kutamba katika mchuano wa mzunguko wa kwanza, ambao wenyeji walitawala kwa zaidi ya asilimia 70 hasa katika kipindi cha pili.

Wenyeji ndio walioanza kupata mabao kupitia Arjen Robben katika dakika ya 11 ya mchuano huo lakini Alexis Sánchez akaisawazishia timu yake katika dakika ya 30, na timu zote zikatoshana nguvu hadi kufikia kipindi cha mapumziko.

Hata hivyo, mambo yalikuwa mabaya sana kwa Arsenal kipindi cha pili baada ya Bayern Munich kureja kwa nguvu na kufunga mabao manne.

Mabao hayo yalitiwa kimyani na Robert Lewandowski, Thiago Alcântara aliyefunga mabao mawili huku Thomas Muller akimaliza kazi katika dakika ya 88 na kufanya mambo kuwa mabao 5-1 hadi kumalizika kwa mchuano huo.

Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amekiri kuwa vijana wake walilemewa katika kipindi cha pili cha mchuano huo na kueleza kuwa, kilichotokea hakiwezi hata kuelezeka.

Arsenal kufuzu ni kuifunga Bayern Munich angalau mabao 5-0 ili kitu ambacho wachambuzi wa soka wanaona kuwa sio rahisi.

Bao la Karim Benzema katika mchuano dhidi ya Napoli. Real Madrid 3-1 Napoli
Bao la Karim Benzema katika mchuano dhidi ya Napoli. Real Madrid 3-1 Napoli Reuters / Susana Vera Livepic

Mbali na mchuano huu, Real Madrid ya Uhispani nayo ilitoka nyuma na kuishinda Napoli ya Italia mabao 3-1.

Mabao ya Madrid yalifungwa na Carlos Casimirio, Karim Benzema na Toni Kross huku Napoli ikipata bao lake la pekee kupitia, Lorenzo Insigne.

Michuano ya mwondoano hatua ya 32 bora nayo inaanza kuchezwa siku ya Alhamisi katika viwanja mbalimbali barani Ulaya.

Ratiba

  • Atletico vs Apoel
  • Manchester United vs Saint-Etiene
  • Villareal vs Roma
  • Gent vs Tottenham Hotspurs
  • Celta Vigo vs Shakhtar Donestsk
  • Krasnodar vs Fenerbahce