NEYMAR-BARCELONA

Mshambuliaji wa Barcelona, Neymar kushtakiwa kwa makosa ya rushwa

Mshambuliaji wa FC Barcelona, Neymar, ambae anakabiliwa na mashtaka ya rushwa nchini Uhispania
Mshambuliaji wa FC Barcelona, Neymar, ambae anakabiliwa na mashtaka ya rushwa nchini Uhispania REUTERS/Vincent West

Mshambuliaji wa kimataifa wa Brazili anayekipiga na klabu ya FC Barcelona ya nchini Uhispania, Neymer, yeye pamoja na klabu yake watapandishwa kizimbani wakikabiliwa na mashtaka ya rushwa kuhusiana na uhamisho wake kutoka klabu ya nchini Brazil ya Santos, baada ya kushindwa kwenye rufaa yake ya awali.

Matangazo ya kibiashara

Kesi dhidi ya Neymer inatokana na malalamiko yliyowasilishwa na kampuni ya nchini Brazil ya DIS ambayo ilikuwa inamiliki asilimia 40 ya haki za mchezaji huyo kuuzwa.

Kampuni hiyo inadai kuwa ilipokea hela pungufu kuliko kiwango ambacho ilistahili kulipwa kutokana na mauzo ya Neymer kwenda kujiunga na klabu ya Barcelona kutoka klabu ya Santos kwa dau la paundi milioni 49 mwaka 2013.

Klabu ya Santos, Neymer mwenyewe, mama yake na kampuni ya mchezaji huyu mwenye umri wa miaka 25 inayomilikiwa na familia yake, wote wanakabiliwa na mashtaka hayo.

Taarifa ya mahakama kuu imesema kuwa "Klabu ya Santos, Barcelona, Neymer, mama yake Nadine Goncalves na kampuni ya N&N ambayo ni kampuni ya familia, wameshindwa kwenye rufaa yao ya mashtaka ya rushwa na udanganyifu".

Kwa uamuzi huu, mchezaji huyo na wahusika wengine wote hawawezi kukata rufaa.

Waendesha mashtaka nchini Uhispania, wanaomba mahakama imuhukumu kifungo cha miaka miwili jela Neymer pamoja na kulipa kiasi cha paundi milioni 8.

Hata hivyo, hata kama mshambuliaji huyu wa Kibrazil atahukumiwa kwenda jela, uwezekano wa yeye kwenda jela ni mdogo sana kutokana na sheria za ulipaji kodi za Uhispania, kuruhusu kifungo hicho kuahirishwa kwa kuwa kipo chini ya miaka miwili.

Waendesha mashtaka pia, wanataka klabu yake ya Barcelona ilipe kiasi cha paundi milioni 7.2 na klabu ya Santos ilipe kiasi cha paundi milioni 5.6.