LA LIGA

Real Madrid yarejea kileleni, Barcelona yaifukuzia kwa karibu, Messi na Morata mashujaa wa timu zao

Wachezaji wa timu ya Real Madrid wakishangilia bao lao la ushindi lililofungwa na Morata katika ushindi wa mabao 3-2.
Wachezaji wa timu ya Real Madrid wakishangilia bao lao la ushindi lililofungwa na Morata katika ushindi wa mabao 3-2. REUTERS/Heino Kalis

Timu ya Real Madrid ya nchini Uhispania usiku wa kuamkia Jumatatu Februari 27, ililazimika kutumia nguvu ya ziada kutoka nyuma kwa mabao mawili kwa bila na kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya klabu ya Villarreal na kurejea kwenye kilele cha ligi kuu ya Uhispania, La Liga.

Matangazo ya kibiashara

Hatua muhimu ilikuwa ilikuwa wakati Villareal inaongoza kwa mabao 2-1 ambapo mchezaji wa Villareal Bruno aliunawa mpira kwenye eneo la hatari, ingawa ilijadiliwa kwa kina ikiwa aliunawa mpira ule kwa makusudi.

Winga Christiano Ronaldo aliisawazishia timu yake bao kupitia mkwaju wa penalt na kufanya matokeo kuwa sare ya mabao 2-2, ambapo bao la kwanza likifungwa na mshambuliaji Gareth Bale.

Mchezaji aliyeingia kipindi cha pili, Alvaro Morata aliipatia timu yake bao la ushindi zikiwa zimesalia dakika 7 pekee mchezo kumalizika.

Madrid sasa ina alama 55, alama moja zaidi mbele ya Barcelona ambayo iliwafunga mahasimu wao klabu ya Atletico Madrid kwa mabao 2-1 mapema siku ya Jumapili ambapo wako kwenye nafasi ya pili kwa alama 52.

Mshambuliaji mu Argentina Lionel Messi aliifungia timu yake bao la ushindi katika dakika za lala salama, na kuisaidia Barcelona kuchomoza na ushindi dhidi ya Atletico Madrid.

Bao la kwanza la Barcelona lilifungwa na mchezaji Rafinha akitumia mpira uliokuwa umepigwa na Luis Suarez.

Hata hivyo mchezaji Diego Godin aliisawazishia timu yake akipokea pasi kutoka kwa mchezaji Koke.