FB BARCELONA

Kocha wa Barcelona, Luis Enrique kung'atuka mwisho wa msimu huu

Kocha mkuu wa klabu wa FC Barcelona, Luis Enrique ambaye ametangaza kuwa ataachia ngazi mwishoni mwa msimu.
Kocha mkuu wa klabu wa FC Barcelona, Luis Enrique ambaye ametangaza kuwa ataachia ngazi mwishoni mwa msimu. Reuters / Christian Hartmann Livepic

Kocha mkuu wa klabu ya FB Barcelona, Luis Enrique, ataachia ngazi kwenye nafasi yake mwishoni mwa msimu huu, akisema anahitaji kupumzika.

Matangazo ya kibiashara

Enrique mwenye umri wa miaka 46, yuko katika msimu wake wa tatu akikinoa kikosi cha Barcelona, amesema haya baada ya mechi ya ligi ambapo timu yake ilichomoza na ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya Sporting Gijon.

Kocha huyu alishinda mataji matatu mfululizo katika msimu wake wa kwanza na FB Barcelona ambapo alitwaa taji la klabu bingwa Ulaya na mataji mawili ya ligi na lile la La Liga.

Hata hivyo Barcelona iko kwenye hatihati kubwa ya kuondolewa kwenye michuano ya klabu bingwa Ulaya baada ya kupoteza kwenye mchezo wake na timu ya PSG ya Ufaransa kwa mabao 4-0 hatua ya 16 bora.

Wachezaji wa FC Barcelona wakishangilia moja ya mataji waliyowahi kushinda chini ya Luis Enrique.
Wachezaji wa FC Barcelona wakishangilia moja ya mataji waliyowahi kushinda chini ya Luis Enrique. REUTERS

Enrique anasema "ni ngumu, ila nimepima na kutafakari sana na nafikiri napaswa kuwa mtiifu kwa kile ninachofikiri," alisema kocha huyo ambaye ataondoka baada ya mkataba wake kumalizika mwishoni mwa msimu.

Kocha huyu ambaye pia ni kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Uhispania, aliichezea Barcelona mwaka 1996 na kustaafu soka mwaka 2004.

Baada ya kustaafu alianza kufundisha kikosi cha timu B kuanzia mwaka 2008 hadi 2011, na kisha kurejea kwenye kikosi cha kwanza kama kocha, akiwa tayari ameshawahi kufundisha vilabu vya AS Roma na Celta Vigo.