KLABU BINGWA ULAYA

Timu ya FC Barcelona yaweka historia michuano ya klabu bingwa Ulaya

Wachezaji wa FC Barcelona wakishangilia baada ya mchezo wao na PSG ambapo wameweka historia kwenye michuano hiyo. Machi 8, 2017.
Wachezaji wa FC Barcelona wakishangilia baada ya mchezo wao na PSG ambapo wameweka historia kwenye michuano hiyo. Machi 8, 2017. Reuters / Albert Gea Livepic

Klabu ya FC Barcelona ya nchini Uhispania imeweka historia kwenye michuano ya klabu bingwa barani Ulaya na kuwa timu ya kwanza kugeuza matokeo ya awali ya mabao 4-0, ambapo imefanikiwa kuiondoa klabu ya PSG ya Ufaransa na kutinga hatua ya robo kwa msimu wa 10 mfululizo.

Matangazo ya kibiashara

Mabingwa hao wa Uhispania walikuwa nyuma kwa tofauti ya mabao 5-3 katika dakika ya 88, lakini wakafunga mabao matatu kwenye dakika saba za mwisho, katika mchezo wa kihistoria kuwahi kutokea.

Bao la penalty na lile la faulo lililofungwa na mshambuliaji Mbrazil Neymer na lile la dakika za lala salama la Sergi Roberto la dakika ya 95 lilifanikisha ushindi wa aina yake kwa mabingwa hao kwenye dimba la Nou Camp.

Barcelona waliongoza kwa mabao 2-0 shukrani kwa bao la Luis Suarez katika dakika ya tatu tu ya mchezo na lile bao la kujifunga la Layvin Kurzawa lilionesha dhahiri dhamira ya FC Barcelona.

Mshambuliaji wa PDG Edison Cavani aliifungia timu yake bao katika dakika ya 61 ya mchezo na kuinua tena matumaini ya timu yake kusonga mbele kwenye hatua ya robo fainali, lakini hata hivyo walishindwa kabisa kuwamudu Barcelona waliofanya mashambulizi ya aina yake na kuchomoza na ushindi.

Katika mchezo mwingine klabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani nayo ilifanya kweli kwa kubadili matokeo ya awali ya bao 1-0 dhidi ya Benfica.

Mabao matatu ya Pierre-Emeric Aubameyang yalitosha kuzamisha jahazi la Benfica kwa jumla ya mabao 4-0 kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya klabu bingwa barani Ulaya.