CAF-MISRI

Rais wa Caf Issa Hayatou na katibu mkuu wake washtakiwa nchini Misri kwa ubadhilifu

Mwendesha mashtaka wa Misri, amepeleka shauri dhidi ya rais wa shirikisho la soka barani Afrika, CAF, Issa Hayatou, kwenye mahakama ya uchumi kuhusiana na mashtaka ya kukiuka sheria za ushindani za ndani ya nchi.

Rais wa shirikisho la mpira barani Afrika, Caf, Issa Hayatou
Rais wa shirikisho la mpira barani Afrika, Caf, Issa Hayatou Cafonline.com
Matangazo ya kibiashara

Katibu mkuu wa Caf, Hicham El Amrani pia ameshtakiwa, huku mawakili wanaowawakilisha wakihudhuria mahakani siku ya Jumatatu.

Huku makao makuu ya Caf yakiwa ni jijini Cairo, mamlaka nchini Misri zinasema taasisi hiyo iko chini ya sheria za nchi hiyo.

Hata hivyo kupitia kwenye mkutano wa kamati ya utendaji uliofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia Jumanne ya Machi 14, imeendelea kupinga madai hayo na kusisitiza kuwa sheria zote zilifuatwa wakati ikitiliana saini mkataba wa mamilioni ya fedha na kampuni ya michezo ya Lagarder mwezi Juni mwaka 2015.

Kamati hiyo inasema itapambana kwa nguvu zote kulinda hadhi yake.

Mamlaka ya ushindani nchini Misri ilianza kuchunguza mkataba wa Caf na kampuni ya Lagardere mwezi Juni mwaka 2016, ikisema kuanzia mwezi Januri mwaka 2017, Caf ilianza kumiliki kibinafsi mkataba huo kinyume cha sheria.

Mkataba huu unaipa kampuni ya Lagardere haki ya michuano mbalimbali barani Afrika, ikiwemo ile mikubwa ya kombe la mataifa ya Afrika kuanzia mwaka 2017 hadi mwaka 2028.

"Kufuatia matokeo haya, bodi ya ushindani ilipiga kura kuunfa mkono suala la Hayatou na katibu mkuu El Amrani lipelekwe kwa mwendesha mashtaka wa makosa ya jinai." ilisema taarifa ya bodi ya ushindani ya Misri.

Caf inasisitiza kuwa tuhuma kuwa iliuza haki hizo bila kutangaza tenda kwa mujibu wa sheria za Misri, haziko sahihi.

Hatua hii inakuja wakati ambapo Alhamisi ya Machi 16, shirikisho hilo litafanya uchaguzi mkuu wake, ambapo Issa Hayatou anawania kuchaguliwa tena.