CAF

Hatma ya Hayatou Caf kujulikana Ahmad Ahmad ampa wakati mgumu

Issa Hayatou, rais wa shirikisho la soka barani Afrika, CAF.
Issa Hayatou, rais wa shirikisho la soka barani Afrika, CAF. FABRICE COFFRINI / AFP

Shirikisho la soka barani Afrika, Caf, Alhamisi hii linafanya uchaguzi wake mkuu, uchaguzi ambao utashuhudia kinyang'anyiro kikali kati ya rais wa sasa Issa Hayatou na rais wa chama cha soka cha Madagascar, Ahmad Ahmad.

Matangazo ya kibiashara

Uchaguzi wa mwaka huu unaelezwa kuwa uchaguzi wa kipekee kutokana na kile wachambuzi wa soka la Afrika wanasema kuwa ni upinzani kutoka kwa Ahmad Ahmad anayeoonekana kuungwa mkono na watu wengi.

Ahmad ambaye tayari amepata uungwaji mkono kutoka kwa viongozi wa mashirikisho maarufu ya Soka barani Afrika, akiwemo rais wa NFF nchini Nigeria, Zimbabwe, Afrika Kusini na baraza la vyama vya soka la nchi za kusini mwa Afrika COSAFA.

Ahmad anasema kuwa ikiwa atachaguliwa kushika nafasi hiyo, ataleta mabadiliko makubwa kwenye shirikisho la mpira Afrika pamoja na kubadili taswira ya soka la Afrika, ahadi ambayo ameonekana kuwashawishi walio wengi.

Kwa upande wake Issa Hayatou ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 29 toka mwaka 1988, anasisitiza kuwa yeye ndie kiungo muhimu kwa soka la Afrika na kwamba nchi nyingi zimenufaika na utawala wake.

Hayatou anawania nafasi hii huku akikabiliwa na kashfa lukuki za ubadhirifu wa mali za CAF, na juma hili mwendesha mashtaka wa Misri aliwasilisha kesi dhidi yake na katibu mkuu, kwenye mahakama ya uchumi.

Katika hatua nyingine wakati wa mkutano wa kamati ya utendaji ya shirikisho hilo, iliridhia kuendelea na shauri la kimaadili dhidi ya rais wa chama cha soka cha Zimbabwe, Phillip Chiyangwa ambaye aliingia kwenye vita ya maneno na Hayatou.