LIGI YA MABINGWA ULAYA

Leicester City kucheza na miamba ya Uhispania Atletico Madrid, Real uso kwa uso na Bayern

Nahodha na beki wa klabu ya Leicester City, Wes Morgan akishangilia na kipa wake Kasper Schmeichel baada ya kufuzu hatua ya robo fainali ya UEFA
Nahodha na beki wa klabu ya Leicester City, Wes Morgan akishangilia na kipa wake Kasper Schmeichel baada ya kufuzu hatua ya robo fainali ya UEFA Reuters / Darren Staples

Shirikisho la soka barani Ulaya UEFA hatimaye limeweka wazi ratiba ya mechi za robo fainali ya michuano ya klabu bingwa Ulaya, ambapo klabu ya Leicester City ya Uingereza imepangwa kucheza na Atletico Madrid ya Uhispania.

Matangazo ya kibiashara

Mabingwa hawa wa ligi kuu ya Uingereza, walifanikiwa kutinga kwenye hatuja ya robo fainali ya michuano ya mwaka huu, baada ya kuwafunga Sevilla kwa jumla ya mabao 3-2.

Leicester watacheza mchezo wao wa kwanza wakiwa ugenini tarehe 12 ya mwezi Aprili, huku mchezo wa marudiano ukitarajiwa kuwa Aprili 18.

Mabingwa watetezi wa kombe hili klabu ya Real Madrid yenyewe imepangiwa kucheza na Bayern Minich ya Ujerumani wakati Barcelona wenyewe watacheza na Juventus ya Italia huku Borussia Dortmund wakicheza na Monaco.

Atletico Madrid ndio timu pekee iliyosalia kwenye hatua hii ya robo fainali ambayo klabu ya Leicester imeshawahi kucheza, lakini mabingwa hawa wa Uingereza hawajawahi kuwafunga wahispania hawa kwenye mechi zao nne zilizopita ambapo walikutana.

Kikosi cha kocha Diego Simeone kilifungwa na Real Madrid kwenye mchezo wa fainali kwa mikwaju ya Penalt.

Atletico wako kwenye nafasi ya nne ya msimamo wa jedwali la timu zinazoshiriki ligi kuu ya Uhispania, La Liga.

Ratiba Kamili:

Atletico Madrid (Uhispania) v Leicester City (Uingereza)

Borussia Dortmund (Ujerumani) v Monaco (Ufaransa)

Bayern Munich (Ujerumani) v Real Madrid (Uhispania)

Juventus (Italia) v Barcelona (Uhispania)