RIADHA-MBIO ZA NYIKA

Chipukizi Jacob Kiplimo aishindia Uganda medali ya kwanza ya dhahabu

Jacob Kiplimo bingwa wa  duniani wa mbio za Kilomita nane kwa chipukizi
Jacob Kiplimo bingwa wa duniani wa mbio za Kilomita nane kwa chipukizi /www.iaaf.org

Mwanariadha chipukizi wa Uganda, Jacob Kiplimo ameweka historia kwa kuishindia nchi yake medali ya dhahabu katika mbio za Nyika za dunia za kilomita nane kwa upande wa wanaume.

Matangazo ya kibiashara

Kiplimo alishinda mbio hizo kwa muda wa dakika 22 na sekunde 40, katika uwanja wa nyumbani wa Kololo jijini Kampala.

Kilomita tatu kabla ya kumaliza mbio hizo zilizoshindaniwa kati ya wanariadha wa Kenya, Ethiopia na Uganda, Kiplimo aliwapita na kuongeza mwendo hadi mwisho.

Ushindi huu umeshangiliwa na maelfu ya raia wa Uganda akiwemo rais Yoweri Museveni aliyekuwa uwanjani kushuhudia mashindano haya.

Hii ndio mara ya kwanza kwa Uganda kupata medali ya dhahabu katika mbio hizi kwa upande wa wanaume chipukizi.

Serikali ya Uganda, ilikuwa imeahidi kuwa mwanariadha yeyote wa nchi hiyo atakayepata medali katika mashindano yoyote ya Kimataifa, atalipwa Shilingi za nchi hiyo Milioni 5 kila mwezi.

Nafasi ya pili ilimwendea Mwiethiopia Amdework Walelegn aliyemaliza kwa muda wa dakika 22 na sekunde 43.

Mkenya Richard Yator Kimunyan alimaliza katika nafasi ya tatu na kujinyakulia medali ya shaba kwa muda wa dakika 22 na sekudne 52.

Kwa upande wa wanawake chipikuzi, Mwiethiopia Letesenbet Gidey ameshinda medali ya dhahabu katika mbio za Kilomita sita.

Akikimbia kwa kujiamini mbio hizo, Gidey alishinda kwa muda wa dakika dakika 18 na sekunde 34 na kutetea taji aliloshinda mwaka 2015 nchini China.

Nafasi ya pili ilimwendea Hawi Feysa pia kutoka Ethiopia aliyemaliza mbio hizo kwa muda wa dakika 18 na sekunde 57.

Mkenya Celliphine Chepteek Chepsol alishinda medali ya shaba kwa kumaliza wa tatu kwa muda wa dakika 19 na sekunde 2.

Mganda mwingine Victor Kiplagat alimaliza katika nafasi ya 18 huku Mtanzania Francis Damiano akimaliza katika nafasi ya 26.

Wanariadha 103 walishiriki katika mbio hizi.