CAF

Katibu mkuu wa shirikisho la soka Afrika CAF Hicham El Amrani ajiuzulu nafasi yake

Rais mpya wa shirikisho la soka barani Afrika Caf, Ahmad Ahmad akizungumza mjini Addis Ababa baada ya ushindi wake. 16 Machi 2017.
Rais mpya wa shirikisho la soka barani Afrika Caf, Ahmad Ahmad akizungumza mjini Addis Ababa baada ya ushindi wake. 16 Machi 2017. REUTERS/Tiksa Negeri

Katibu mkuu wa shirikisho la soka barani Afrika CAF, Hicham El Amrani ametangaza kujiuzulu wadhifa wake mwishoni mwa juma bila ya kutoa maelezo ya sababu za kufikia uamuzi wake.

Matangazo ya kibiashara

Amrani mwenye umri wa miaka 37 raia wa Morocco, ametangaza uamuzi wake kupitia kwenye barua yake aliyoliandikia shirikisho la mpira barani Afrika, CAF.

Hata hivyo wadadisi wa mambo wanaona kuwa kujiuzulu kwake kuna uhusiano mkubwa na kuanguka kwa aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu kwenye shirikisho hilo, Issa Hayatou, aliyeangushwa na Ahmad Ahmad rais wa chama cha soka cha Madagascar.

Katibu mkuu huyo alikuwa kiongozi mtiifu kwa Hayatou na mara kadhaa amekuwa akimtetea Hayatou aliyeliongoza shirikisho hilo kwa miaka 29.

Hicham alikuwa katibu mkuu wa muda mwaka 2010 baada ya aliyekuwa katibu mkuu Mustapha Fahmy kupelekwa shirikisho la kabumbu la dunia Fifa.

Rais mpya wa CAF, Ahmad Ahmad tayari amechukua rasmi ofisi kutoka kwa Issa Hayatou mwishoni mwa juma, ambapo hii leo atakuwa na mkutano na maofisa wa shirikisho la CAF mjini Cairo.

Rais mpya wa CAF anaonekana hata kuwa kipenzi na rafiki wa karibu wa rais wa Fifa, Gianni Infantino ambaye toka awali alionekana kumuunga mkono na hata kufanya ziara kadhaa kwenye mataifa ya Afrika kujaribu kuwashawishi viongozi wamchague.

Ahmad ambaye wakati wa kampeni zake aliahidi kufanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji kwenue shirikisho hilo, anatajwa kama mtu makini ambaye huenda akabadili sura ya kiutendaji ya shirikisho hilo.