AFCON 2019

Timu ya taifa ya soka ya Kenya yaendelea kuimarika kwa kutoshindwa mechi 10 za Kimataifa

Timu ya taifa ya soka ya Kenya, Harambee Stars.
Timu ya taifa ya soka ya Kenya, Harambee Stars. youtube

Timu ya taifa ya soka ya Kenya Harambee Stars haijashindwa katika mechi 10 za Kimataifa ilizocheza tangu mwezi Mei mwaka 2016.

Matangazo ya kibiashara

Haya ni mafanikio makubwa kwa kocha Stanley Okumbi ambaye amekuwa mkufunzi wa timu hiyo mwezi Februari mwaka 2016.

Mafanikio ya Kenya yalianza kushuhudiwa baada ya Harambee Stars kutoka sare ya bao 1-1 na Taifa Stars ya Tanzania katika mchuano wa Kimataifa wa kirafiki.

Hali ilikuwa hivyo dhidi ya Sudan jijini Nairobi lakini pia ikaendelea kuonesha mafanikio baada ya kuishinda Congo Brazaville mabao 2-1 katika mchuano muhimu wa kufuzu kucheza fainali ya bara Afrika nchini Gabon, lakini kwa bahati mbaya haikufanikiwa kufuzu.

Uganda iliikaribisha Kenya katika mchuano wa kirafiki mwezi Agosti mwaka 2016 katika uwanja wa Namboole na kutoka sare ya kutofungana jijini Kampala.

Mabingwa wa bara Afrika mwaka 2012 Zambia , walipata pigo baada ya Kenya kulazimisha sare ya bao 1-1 mjini Ndola katika mchuano wa kufuzu kwenda AFCON mwaka 2017 nchini Gabon.

Matokeo mengine, michuano ya Kimataifa ya kirafiki:-

  • DR Congo 0–1 Kenya
  • Kenya 1-0 Msumbiji
  • Kenya 1-0 Liberia
  • Uganda 1- 1 Kenya
  • DR Congo 1- 2 Kenya

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Kenya iliifunga DRC mabao 2-1 katika mchuano wa Kimataifa wa kirafiki uliopigwa katika uwanja wa Kenyatta mjini Machakos.

Matokeo haya yameendelea kuwafanya mashabiki wa soka nchini Kenya kuanza kujenga imani na kocha Okumbi ambaye hawakumwamini alipoteuliwa.

Wengi walidai kuwa hakuwa na uzoefu wowote lakini, matokeo haya yanatoa picha nyingine kuhusu ukufunzi wake.

Wachambuzi wa soka wanasema sasa kazi kubwa kwa Okumbi ni kufuzu kwa fainali ya kombe la bara Afrika mwaka 2019 nchini Cameroon.

Kenya imepangwa pamoja na Ghana, Sierre Leone na Ethiopia.

Kikosi cha sasa cha Harambee Stars:- Bonface Oluoch, Jockins Otieno, Brian Mandela, David Owino, Abud Omar, David Ochieng, Johanna Omollo, Samuel Onyango, Jesse Were, Michael Olunga.