TENNIS

Jeraha lamweka nje Andy Murray katika robo fainali ya kuwania taji la Davis

Bingwa nambari moja duniani katika mchezo wa Tennis kwa upande wa wanaume Mwingereza Andy Murray, hataweza kuichezea timu yake ya taifa katika mchuano wa robo fainali dhidi ya Ufaransa kuwania taji la Davis.

Andy Murray
Andy Murray Reuters/Paul Childs
Matangazo ya kibiashara

Mchuano huo utachezwa nchini Ufaransa mwezi Aprili kati ya tarehe 7 na 9 mjini Rouen.

Kutokuwepo kwa Murray anayeuguza jeraha la kisugudi cha mkono, ni pigo kubwa kwa timu ya taifa ya Uingereza ambayo ilikuwa inamtegema Murray kufuzu katika hatua ya nusu fainali.

Murray ni mchezaji ambaye amekuwa akitegemewa sana kutokana na ushupavu wake lakini pia kutokana na rekodi ya ubingwa mara tatu wa mashindano makubwa duniani lakini pia michezo ya Olimpiki.

Nahodha wa Uingereza Leon Smith amekiri kuwa watamkosa sana Murray lakini kikubwa ni kumtakia nafuu ya haraka ili arejee uwanjani.

Mbali na mchuano kati ya Uingereza na Ufaransa, Ubelgiji itakuwa nyumbani kumenyana na Italia, huku Australia ikimenyana na Marekani.

Mjini Belgrade, Serbia itamenyana na Uhispania katika mchuano mwingine wa robo fainali.

Bingwa mtetezi wa taji hili ni timu ya taifa ya Argentina.

Haya ni makala ya 106 ya mashindano haya yanayoshirikisha timu za wanaume za wachezaji watano kila upande.

Mashindano haya huchezwa kati ya mwezi Februari hadi Novemba kila mwaka.

Mataifa zaidi ya 100 hushiriki katika hatua mbalimbali ya mwondoano katika michuano ambayo wanasema ndio kombe la dunia la mchezo huu.