ARSENAL

Wenger asema Arsenal inaweza kumaliza katika nafasi ya nne bora

Kocha wa Arsene Wenger
Kocha wa Arsene Wenger Reuters/Michael Dalder

Kocha wa klabu ya Arsenal nchini Uingereza Arsene Wenger, amesema jitihada zinazofanywa na wachezaji wake kuhakikisha kuwa klabu hiyo inamaliza katika nafasi ya nne bora msimu huu, sio kazi rahisi kama wengi wanavyofikiria.

Matangazo ya kibiashara

Kauli hii ya Wenger imekuja akiendelea kuwa na historia ya kuhakikisha kuwa Arsenal inamaliza katika nne bora na kufuzu katika michuano ya klabu bingwa barani Ulaya kwa kipindi chote cha miaka 20 ambacho amekuwa kocha wa klabu hiyo.

Raia huyo wa Ufaransa amesema licha ya ligi ya Uingereza kuwa na ushindani mkali, anaamini kuwa klabu yake itamaliza katika nne bora msimu huu.

Mwaka 2012, baada ya klabu yake kumaliza katika nafasi za nne bora, Wenger alisema hatua hiyo ni kama kushinda ligi kuu ya soka nchini humo kutokana na ushindani mkali katika ligi hiyo.

Arsenal siku ya Jumatano itakuwa nyumbani kimenyana na West Ham United, kutafuta alama tatu muhimu.

Baada ya kucheza mechi 28, Arsenal kwa sasa inashikilia nafasi ya 6 kwa alama 51, nyuma ya Manchester United ambayo ina alama 53.

Chelsea inaongoza kwa alama 69.

Tottenham Hotspurs ni ya pili kwa alama 62, Liverpool ya tatu kwa alama 59 huku Manchester City ikiwa ya nne kwa alama 58.