NDONDI-JOSHUA-KLITCHKO

Mabondia Anthony Joshua na Wladimir Klitschko kukata mzizi wa fitina

Anthony Joshua (kushoto) na Wladimir Klitschko ambao watapokea kitita cha dola milioni 13 baada ya pambano lao la April 29, 2017.
Anthony Joshua (kushoto) na Wladimir Klitschko ambao watapokea kitita cha dola milioni 13 baada ya pambano lao la April 29, 2017. Reuters/Andrew Couldridge

Mashabiki na wapenzi wa masumbwi duniani usiku wa Jumamosi April 29 watashuhudia mpambano wa masumbwi wa aina yake kati ya bondia Muingereza Anthony Joshua na mu Ukraine Wladimir Klitschko, mabondia hawa wakiwania taji la dunia la uzito wa juu.

Matangazo ya kibiashara

Wanamasumbwi hawa watapambana kwenye uwanja wa Wembley, ambapo kabla hata ya pambano lenyewe bondia Joshua amejinasibu kumuangusha mpinzani wake kwenye raundi ya kwanza ya pambano lao.

Hili linatajwa kuwa pambano kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa kwenye miaka ya hivi karibuni, ambapo mashabiki wa mchezo huo zaidi ya elfu 90 wanatarajia kulishuhudia.

Kwa upande wake bondia Klitschko amejirekodi kupitia picha ya video akitabiri matokeo ya pambano lao, akiihifadhi video hiyo kwenye kamba ya bukta yake ambayo ataivaa wakati wa pambano lake.

Baada ya mechi bondia huyo anataraji kuiuza flash aliyohifadhia video aliyojirekodi sambamba na nguo zake alizokuwa amevaa kabla ya pambano kwaajili ya kukusanya fedha za kusaidia kituo chake cha misaada.

Klitschko amesema “najiona kwa AJ (Joshua), najua anawaza nini, ataenda kufanya nini na namna pambano litakavyokuwa. Lakini mimi si mtoto wa Nostradamus, lakini najisikia mwenye nguvu sana kwa nnachokifanya,” alisema bondia huyo mwenye umri wa miaka 41.

Kwa upande wake Joshua mwenye umri wa miaka 27 amesema hata potezwa maboya na matamshi ya mpinzani wake akisema ni uongo! Na watu wasubiri waone atakachomfanya mpinzani wake.

Kwenye pambano hili mikanda kadhaa ya Joshua atakuwa akiitetea likiwemo taji la IBF na lile lililo wazi la WBA.

Kila bondia anatarajia kuvuna kitita cha paundi milioni 10 ambacho ni sawa na dola milioni 13 na euro milioni 12.