KOMBE LA DUNIA-SOKA

Guinea yalazimisha sare dhidi ya Uingereza michuano ya kombe la dunia kwa vijana

Uingereza ikimenyana na Guinea katika mchuano wa pili wa kombe la dunia kwa vijana Mei 23 2017
Uingereza ikimenyana na Guinea katika mchuano wa pili wa kombe la dunia kwa vijana Mei 23 2017 FIFA.COM

Timu ya taifa ya soka ya Guinea ya vijana chini ya umri wa miaka 20, imepata alama  ya kwanza katika michuano ya kombe la dunia inayoendelea nchini Korea Kusini.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hii ilikuja baada ya vijana hao kulazimisha sare ya bao 1-1 na Uingereza katika mchuano wake wa pili wa kundi A.

Uingereza ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya 53, lakini ikajifunga katika dakika nne baadaye na kuizawadia Guinea bao.

Guinea ilianza vibaya mwishoni mwa wiki iliyopita, baada ya kufungwa na wenyeji wa michuano hii Korea Kusini mabao 3-0.

Licha ya sare hii, Uingereza ambayo ilishinda mechi yake ya kwanza dhidi ya Argentina kwa mabao 3-0, inaendelea kuongoza kundi hilo kwa alama 4.

Venezuela nayo imeendelea kuongoza kundi la B kwa alama 6 baada ya kushinda mechi yake ya pili siku ya Jumanne kwa kuichabanga Vanuatu mabao 7-0.

Wawakilishi wengine wa Zambia ambao wamepangwa katika kundi la C, itamenyana na Iran katika mchuano wake wa pili hapo kesho.

Mechi ya kwanza, Zambia ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ureno na sasa inaongoza kwa alama 3.

Senegal nayo ilianza vema katika kundi la D hapo jana kwa kuishinda Saudi Arabia mabao 2-0. Mechi ya pili itakuwa kati ya Marekani siku ya Alhamisi.

Afrika Kusini ambayo ipo katika kundi D, ilianza vibaya baada ya kufungwa na Japan mabao 2-1 wiki iliyopita.

Mataifa 24 kutoka mabara 6 yanashiriki katika michuano hii, itakayomalizika tarehe 11 mwezi Juni.

Bara la Afrika linawakilishwa na Guinea, Senegal, Afrika Kusini na Zambia.