SOKA

Zambia yafuzu hatua ya mwondoano kombe la dunia la vijana

Timu ya taifa ya vijana ya Zambia baada ya kufuzu katika hatua ya mwondoano kombe la dunia Mei 24 2017
Timu ya taifa ya vijana ya Zambia baada ya kufuzu katika hatua ya mwondoano kombe la dunia Mei 24 2017 FIFA.COM

Timu ya taifa ya soka yenye wachezaji wasiozidi miaka 20, wamefuzu katika hatua ya mwondoano kutafuta ubingwa wa dunia. 

Matangazo ya kibiashara

Zambia ilifanikiwa kuingia katika hatua hiyo baada ya kushinda mechi yake ya pili ya hatua ya makundi kwa kuilemea Iran mabao 4-2.

Chipolopolo ilitoka nyuma, ikiwa na mabao 2-0 na kusawazisha dhidi ya wapinzani wao katika dakika ya 54 na 59, kipindi cha pili cha mchuano huo uliochezwa katika uwanja wa Jeju mjini Seogwipo.

Walioifungia Zambia ni pamoja na Fashion Sakala dakika ya 54, Enock Mwepu dakika ya 59, Emmanuel Banda dakika 65 na Paston Daka aliyemaliza karamu ya mabao katika dakika ya 71.

Iran ilianza vema kwa kupata bao la mapema kupitia mshambuliaji wake Reza Shekari katika dakika ya 7 na kupitia mikwaju ya penalti dakika ya 49.

Mataifa mengine yaliyofuzu ni pamoja na Korea Kusini ambao ni wenyeji wa michuano hii katika kundi A, na Venezuela kutoka kundi B.

Wawakilishi wengine wa Afrika, Afrika Kusini wamefungwa na Italia mabao 2-0 katika mechi yake ya pili na kudidimiza matumai ya kusonga mbele kwa sababu mechi ya kwanza ilifungwa na Japan kwa mabao 2-1.

Mechi ya mwisho, Afrika Kusini itacheza na Uruguay mwishoni mwa wiki hii.

Wawakilishi wengine wa Afrika ni Guinea na Senegal.

Ratiba ya mechi za Jumatano Mei 24 2017:

  • Costa Rica vs Ureno
  • Uruguay vs Japan