ICC-DRC

Bosco Ntaganda kuanza kujitetea katika Mahakama ya ICC

Aliyekuwa kiongoiz wa waasi nchini DRC Bosco Ntaganda (Kulia) akiongozwa na askari wa Mahakama ya ICC kuingia Mahakamani
Aliyekuwa kiongoiz wa waasi nchini DRC Bosco Ntaganda (Kulia) akiongozwa na askari wa Mahakama ya ICC kuingia Mahakamani AFP PHOTO/ POOL / MICHAEL KOOREN

Aliyekuwa kiongozi wa kundi la waasi la FPLC nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Bosco Ntaganda, hatimaye atatoa ushahidi wa kujitetea katika Mahakama ya Kimataifa ya ICC siku ya Jumatano.

Matangazo ya kibiashara

Ntaganda maarufu kama "The Terminator" amekuwa akikanusha madai kuwa aliwatumia watoto wadogo kama wapiganaji na kuwatumia wanawake na wasichana kama watumwa wa kingono.

Kesi dhidi ya Ntanganda ilianza miaka miwili iliyopita mjini Hague nchini Uholanzi, alipofunguliwa mashtaka ya mauaji katika jimbo la Ituri yaliyotokea kati ya mwaka 2002 na 2003.

Ntaganda mwenye umri wa miaka 43, amekanusha madai yote 13 ya uhalifu wa kivita na mengine matano ya ukiukwaji wa haki za binadamu, yaliyotekelezwa na waasi hao.

Watu zaidi ya 60,000 walipoteza maisha na wengine kuyakimbia makwao baada ya kuvamiwa na waasi hao.

Kabla ya kufikishwa katika Mahakama ya ICC, Ntaganda alijisalimisha katika Ubalozi wa Marekani jijini Kigali  nchini Rwanda mwaka 2013.