FIFA yakataa ombi la Etoile Filante kuizua Cameroon kushiriki fainali ya mabara

Mabingwa wa soka barani Afrika, Cameroon.
Mabingwa wa soka barani Afrika, Cameroon. Cafonline

Shirikisho la soka duniani FIFA, limekataa ombi la klabu ya soka ya Etoile Filante de Garoua kutoka nchini Cameroon , kuizua timu ya taifa kushiriki katika michuano ya mabara itakayofanyika kuanzia tarehe 17 mwezi huu nchini Urusi.

Matangazo ya kibiashara

Klabu ya Etoile Filante inayompinga rais wa Shirikisho la soka nchini humo Tombi Roko Sidiki, imekuwa ikisema kiongozi huyo hana mamlaka ya kuituma timu hiyo ya taifa katika michuano hiyo.

FIFA imesema inafahamu kuwa kuna changamoto ya uongozi katika Shirikisho hilo la FECAFOOT lakini inaendelea kumtambua Sidiki kama kiongozi halali wa Shirikisho hilo.

Aidha, FIFA ambayo iliwahi kuifungia Cameroon kushiriki katika michuano ya Kimataifa mwaka 2013 kwa sababu ya mzozo wa uongozi ndani ya Shirikisho hilo, inaendelea kufanya mazungumzo na wadau wa soka nchini humo kutatua mzozo uliopo.

Cameroon imepangwa katika kundi la B na Chile, Australia na Ujerumani.

Kundi la A lina Urusi, New Zealand, Ureno na Mexico.

Cameroon iliyoshinda taji la bara Afrika mapema mwaka 2017 nchini Gabon, itachuana na Chile tarehe 18 katika uwanja wa Otkytiye Arena jijini Moscow.