DRC-FECOFA

Refarii Azanga Kalamba Justin afungiwa maisha na FECOFA

Polisi wa kuzuia fujo wakipambana na mashabiki wakati wa mchuano wa Sanga Balende na Don Bosco
Polisi wa kuzuia fujo wakipambana na mashabiki wakati wa mchuano wa Sanga Balende na Don Bosco radiookapi.net

Shirikisho la soka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FECOFA) limemfungia maisha mwamuzi wa kati Azanga Kalamba Justin.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hii inakuja baada ya mwamuzi huo kuchezesha mechi ya ligi kuu nchini humo kati ya klabu ya Sanga Balende na Don Bosco , mchuano uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Anakuwa mwamuzi wa tatu kufunguliwa na FECOFA, baada ya uamuzi kama huo kuchukuliwa dhidi ya Claude Kamulete na Bremer Engbanguku.

Mbali na marefarii hao, wafanyikazi wengine wa Shirikisho hilo Delphin Kikuni Makamu Mwenyekiti wa kamati inayosimamia ligi kuu nchini humo na Katibu wake José Konde, wamefungiwa kwa muda wa miezi sita.

FECOFA inasema baada ya uchunguzi wa kina, wamebaini kuwa mwamuzi huyo alishawishi matokeo ya mchuano huo kimakusudi na kuzua fujo uwanjani.

Sanga Balende inashikilia nafasi ya tano kwa alama 14, mbele ya Don Bosco ambayo ina alama 12 baada ya mehi 12 ilizocheza kuwania ubingwa wa ligi kuu msimu huu.

Hata hivyo, ushindani ni kati ya mabingwa watetezii TP Mazembe ambao baada ya mechi 11 inaongoza ligi kwa alama 24, huku mshindani mkubwa akiwa ni DC Motema Pembe ambayo ina alama 21 sawa na AS Vita Club baada ya kucheza mechi 10.

Mechi ya mwisho itakuwa ni kati ya Mazembe dhidi ya AS Vita Club tarehe 14 mwezi Julai, lakini kabla ya hilo, itamenyana na Bukavu Dawa siku ya Jumapili.