TANZANIA-SOKA

Rais wa Shirikisho la soka nchini Tanzania, akamatwa

Rais wa Shirikisho la soka nchini Tanzania Jamal Malinzi
Rais wa Shirikisho la soka nchini Tanzania Jamal Malinzi twitter.com/jamalmalinzi

Rais wa shirikisho la soka nchini Tanzania TFF Jamal Malinzi na Katibu wake Mkuu Celestine Mwesigwa, wameendelea kushikiliwa na kuhojiwa na mamlaka ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini humo TAKUKURU.

Matangazo ya kibiashara

Ripoti zinasema kuwa viongozi hao wanatarajiwa kufikishwa Mahakamani na kufunguliwa mashtaka kwa madai ya matumizi mabaya ya Ofisi.

Vyombo ya Habari nchini Tanzania vinaripoti kuwa wachunguzi wa Mamlaka hayo yanamshikilia Malinzi kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya fedha za kufadhili soka nchini humo.

Duri zinasema kuwa kukamatwa kwao kunahusiana na ukaguzi wa fedha za udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa Taifa Stars iliyotolewa Oktoba 2, 2014, kwa madai kuwa wakuu wa soka nchini humo walikwenda kinyume na makubaliano ya mkataba kati ya pande zote mbili.

Aidha, ripoti hiyo ilibainisha kuwa Kati ya Novemba 11, 2013 na Machi 11, 2014, Dola za Marekani 381,248 zilitolewa kwenye akaunti hiyo na kutumika kwa shughuli ambazo hazijaainishwa katika mkataba wa TBL na TFF.

Malinzi anakabiliwa na changamoto hii wakati huu Uchaguzi wa kumpata rais mpya wa TFF ukitarajiwa kufanyika mwezi Agosti.

Rais huyo ni miongoni mwa wagombea 10 wanaotaka nafasi hiyo.