OLIMPIKI 2024

Miji ya Paris na Los Angeles kuamua mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki 2024

Bendera ya jijini Paris, olimpiki
Bendera ya jijini Paris, olimpiki AFP/Gabriel Bouys

Kamati ya Kimataifa ya Michezo ya Olimpiki imekubali kutoa fursa kwa jiji la Paris nchini Ufaransa na Los Angeles nchini Marekani kuandaa michezo ya Olimpiki mwaka 2024 na 2028.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa Kamati hiyo Thomas Bach amesema miji ya Paris na Los Angeles imepata nafasi ya kipekee kufanikisha michezo hiyo, sasa kazi ni kwa maafisa wa nchi hizo mbili kuamua ni nani atatangulia.

Wawakilishi wa Ufaransa na Marekani wakishirikiana na maafisa wa IOC wana miezi miwili kukubaliana ni mji upi utakuwa wa kwanza kuandaa michezo hii.

Inatarajiwa kuwa kufikia tarehe 13 mwezi Septemba wakati Mkuu wa Kamati ya Olimpiki utakapofanyika jijini Lima nchini Peru, kutakuwa na mwafaka.

Ufaransa imekuwa ikisema inataka kuandaa michezo ya mwaka 2024 wala sio 2028 huku rais Emmanuel Macron akisema Wafaransa wako tayari.

Naye rais wa Marekani Donald Trump kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema, nchi yake infanya bidii kuwa wenyeji wa michezo hiyo bila anapendelea iwe lini.

Marekani ilipata nafasi ya kundaa michezo hiyo kwa mara ya mwisho mwaka 1984.

Ufaransa imekuwa ikijaribu kupata wenyeji wa michezo hiyo mikubwa mara nne, 1992, 2008 na 2012 bila mafanikio.

Mwaka 2020, michezo hii itafanyika jijini Tokyo nchini Japan.

Orodha ya miji iliyowahi kuandaa Michezo hii:-

  • London, Uingereza-1908,1948,2012.
  • Los Angeles, Marekani-1932,1984.
  • Paris, Ufaransa-1900,1924.
  • Athens, Ugiriki-1896, 2004.
  • Beijing, China-2008.
  • Tokyo, Japan-1964.