SOKA-DRC

TP Mazembe na AS Vita Club kupambana Jumatano kutafuta taji la ligi kuu

Wachezaji wa TP Mazembe
Wachezaji wa TP Mazembe TP Mazembe

Bingwa wa soka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo atafahamika siku ya Jumatano wakati mabingwa watetezi TP Mazembe watakapomenyana na AS Vita Club katika mchuano wa mzunguko wa mwisho katika uwanja wa Kamalondo mjini Lubumbashi.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hii imekuja baada ya timu zote mbili kutoshana nguvu kwa alama 30, baada ya mechi 13 kuelekea mzunguko wa mwisho ili kumaliza mzunguko wa 14.

Mbali na timu hizi mbili, timu zingine sita ambazo ni DC Motema Pembe, Don Bosco, Sanga Balende, Muungano, Bukavu Dawa na FC Ranaissance, zimekuwa zikichuana kushinda ligi kuu nchini humo msimu huu.

Kuelekea mchuano huo wa mwisho kati ya Mazembe na AS Vita Club, timu zote mbili zimeshinda mechi tisa, kwenda sare mara tatu na kupoteza mchuano mmoja.

Mshindi siku ya Jumatano ataiwakilisha nchI hiyo katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika msimu ujao, huku mshindi wa pili akicheza katika michuano ya Shirikisho.

DC Motema Pembe ambayo ilikuwa mbioni kutafuta ubingwa msimu huu, itamaliza katika nafasi ya tatu kwa alama 27 baada ya kushinda mechi nane, kwenda sare mechi  tatu na kufungwa michuano mingine mitatu.