TP MAZEMBE

TP Mazembe ndio mabingwa wa ligi kuu ya soka nchini DRC

Mashabiki wa klabu ya TP Mazembe wakisherehekea baada ya kushinda taji la ligi kuu ya soka Julai 19 2017
Mashabiki wa klabu ya TP Mazembe wakisherehekea baada ya kushinda taji la ligi kuu ya soka Julai 19 2017 www.tpmazembe.com

Klabu ya TP Mazembe imeshinda makala ya 22 ya ligi kuu ya soka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hii imekuja baada ya kuifunga klabu ya AS Vita Club ya Kinshasa bao 1-0 katika mchuano wa ligi kuu uliochezwa siku ya Jumatano katika uwanja wa Kamalondo mjini Lubumbashi.

Bao pekee la Mazembe lilifungwa na Daniel Adjei kutoka nchini Ghana katika dakika ya pili ya mchuano huo baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa mchezaji mwenzake Jo Issama Mpeko.

TP Mazembe walioshinda taji hili mwaka uliopita, wamemaliza ligi hiyo kwa alama 33 katika mechi 14 ya mwondoano ilizocheza. Hili ni taji la 16 la klabu hiyo inayomilikiwa na mwanasiasa wa upinzani Moise Katumbi Chapwe.

Miaka ambayo Mazembe imeshinda taji hili ni mwaka, 1966, 1967, 1969, 1976, 1987, 2000, 2001, 2006, 2007, 2009, 2011, 2012, 2013, 2014, 2016 na 2017.

Katumbi anayehudhuria mkutano Mkuu wa CAF nchini Morocco amewapongeza wachezaji wa klabu yake na kusema walicheza kwa kujitoa na kuonesha ushupavu wa hali ya juu.

Vijana wa kocha Pamphile Mihayo sasa watacheza katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika msimu ujao.

Kocha wa AS Vita Club Florent Ibenge amesema klabu yake ilipoteza kwa sababu wachezaji wake walikuwa wachovu baada ya safari ndefu kutoka jijini Kinshasa.

Vita Club sasa itashiriki katika michuano ya Shirikisho barani Afrika mwaka ujao.