UGANDA-SOKA

Makocha zaidi ya 200 waomba kazi kuifunza timu ya taifa ya Uganda

Mchezo wa soka
Mchezo wa soka Reuters

Makocha zaidi ya 200 kutoka nchi mbalimbali duniani wameomba kazi ya kuifunza timu ya taifa ya soka ya Uganda.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hii imekuja baada ya Shirikisho la soka nchini humo kutangaza nafasi ya kumtafuta kocha mpya.

Miongoni mwa makocha waliotuma maombi hayo ni kocha wa muda Moses Basena raia wa Uganda ambaye ameisaidia Uganda Cranes kufuzu katika fainali ya CHAN mwaka 2018 nchini Morocco.

“Nimekuwa kocha msaidizi kwa muda sasa, na niliisaidia Uganda kufuzu katika fainali ya mataifa bingwa barani Afrika nchini Gabon naamini nina uwezo” ameimbia BBC.

Nafasi ya kocha Mkuu katika timu hiyo ya taifa ilisalia wazi baada ya kujiuzulu kwa Mserbia Milutin 'Micho' Sredojevic mwezi Agosti.

Rais wa zamani wa soka nchini Zambia Kalusha Bwalya, anaongoza kamati ya kumtafuta kocha mpya ambaye atatangazwa kufikia tarehe 15 mwezi Novemba.

Mfaransa Claude LeRoy ni miongoni mwa makocha walioomba kazi hiyo na iwapo atapata nafasi hiyo, Uganda itakuwa nchi yake ya saba kufunza soka barani Afrika.

Kocha huyo wa sasa anayefunza soka nchini Togo, amewahi pia kuwa kocha wa Cameroon na kuisadia kunyakua taji la Afrika mwaka 1988.

Le Roy amefunza pia Senegal, Ghana, Congo na DRC kwa nyakati tofauti.

Mreno Joao Miguel de Castro Ferreira, ambaye amefunza soka nchini Ureno na Saudi Arabia, pia ni miongoni mwa makocha waliomba kazi hiyo.