YANGA-SIMBA-TANZANIA

Yanga, Simba zaanza kuwakilisha Tanzania, michuano ya klabu Afrika

Timu za Yanga na Simba ambazo ni wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya ngazi ya klabu barani Afrika, kesho na keshokutwa zinaanza kampeni ya kuwania michuano ya Kombe la klabu bingwa na kombe la shirikisho.

Wachezaji wa klabu ya Simba FC nchini Tanzania
Wachezaji wa klabu ya Simba FC nchini Tanzania allafrica.com
Matangazo ya kibiashara

Jumamosi, Yanga itakuwa mwenyeji wa timu ya St. Louis ya Shelisheli katika mechi ya mkondo wa awali ya itakayochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni. Yanga itamtegemea zaidi msham,buliaji wake kutoka Zambia, Obrey Chirwa ambaye amefunga mabao 10 katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Mchezo wa marudiano baina ya timu hizo utachezwa wiki ijayo nchini Shelisheli.

Kwa upande mwingine, Simba SC ambayo imekosa michezo ya kimataifa kwa misimu mitano, itaanza harakati za kuwania kombe la Shirikisho kwa kuvaana na timu ya Gendarmarie ya Djobout, mchezo utakachezwa Jumapili katika Uwanja wa Taifa.

Simba itamtegemea mshambuliaji wake kutoka Uganda, Emanuel Okwi ambaye amefunga mabao 13 katika ligi kuu ya Tanzania kufikia sasa.

Hata hivyo Simba itamkosa kiungo wake kutoka Rwanda, Haruna Niyonzima ambaye anasumbuliwa na jeraha la mguu.

Wachezaji wengine wanaotarajiwa kukibeba kikosi cha Simba kinachonolewa na Mfaransa Pierre Lechantre ni Shiza Kichuya John Bocco na Jonas Mkude.

Mechi ya mkondo wa pili baina ya Simba na Gendarmarie itachezwa wiki ijayo nchini Djobout.

Ripoti ya Mwandishi wa RFI Kiswahili, Fredrick Nwaka