GHANA-AUSTRALIA-MICHEZO

Australia yawatimua 'waandishi 50' kutoka Ghana kwa kushindwa kujibu maswali ya michezo

Zaidi ya watu 50 kutoka nchini Ghana waliokuwa wakijaribu kuingia nchini Australia wakidai kuwa waandishi wa habari wanaoenda kuripoti habari za mashindano ya madola (Commonwealth games) walikamatwa baada ya kushindwa kujibu maswali rahisi kuhusu michezo.

Mashabiki wa timu ya taifa ya Ghana katika michuano ya Afcon 2017.
Mashabiki wa timu ya taifa ya Ghana katika michuano ya Afcon 2017. RFI/Pierre René-Worms
Matangazo ya kibiashara

Watu hao waliobainika kuwa walijidai kuwa waandishi ili wapate kuingia nchini humo kirahisi walishikiliwa na baadaye kufukuzwa licha ya kuwa na nyaraka zote sahihi za kusafiria.

Duru za polisi zinasema maafisa wa uhamiaji walibaini njama za watu kuingia nchini humo kwa mgongo wa mashindano hayo huku wakiwa na shughuli zao binafsi, hivyo waliandaa maswali ambayo ni ya kawaida kwa watu wanaofuatilia michezo.

Naibu Waziri wa Michezo wa Ghana, Pious Enam Hadidze, amesema kuwa wameanza kufanya uchunguzi kuhusu sakata hilo ili kubaini kama kuna udanganyifu uliofanyika katika kuwapa vibali.