DRC-SOKA-MICHEZO

Rais wa Shirikisho la Soka DRC awekwa chini ya ulinzi

Rais wa Shirikisho la Soka nchini DRC (Fecofa), Constant Omari, na maafisa wengine watatu wa michezo nchini humo wamewekwa chini ya ulinzi mjini Kinshasa. Uamuzi huo umechukuliwa na mahakama kwa kosa la matumizi ya fedha za umma.

uwanja wa mpira wa Tata Raphaël, Kinshasa. Maafisa wanne wa michezo wawekwa chini ya Ulinzi DRC.
uwanja wa mpira wa Tata Raphaël, Kinshasa. Maafisa wanne wa michezo wawekwa chini ya Ulinzi DRC. capture d'écran youtube
Matangazo ya kibiashara

Omari, ambaye pia ni Naibu rais wa Shirikisho la Soka barani Afrika na mwanachama wa kamati tendaji ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA), ameonekana mdhaifu, aliporipoti kwenye ofisi ya mwendesha mashitaka katika wilaya ya Limete, katikati mwa mji wa Kinshasa, kwa mujibu wa mwandishi wa shirika la habari la AFP.

Constant Omari, Barthelemy Okito, Katibu Mkuu wa Michezo nchini DRC, Roger Bondembe na Théobad Binamungu, Manaibu wawili wa rais wa Fecofa, wako "chini ya ulinzi" tangu Jumanne wiki hii na "wanasubiri kusikilizwa," mwendesha mashitaka ambaye hakutaja jina lake ameliambia shirika la habari la AFP.

“Walihojiwa kuhusu matumizi ya fedha za umma katika maandalizi ya michuano ya timu za taifa za soka na klabu zilizoshiriki katika michuano ya Afrika," amesema hakimu.

Watu wanne "walisikilizwa kuhusu madai ya kupitisha mlango wa nyuma dola milioni moja, fedha zilizokua zimetolewa kwa ajili ya maandalizi ya mechi nne za soka ," amesema kwa upande wake wakili Alain Makengo, mwanasheria wa wanasoka wa DRC.