FC BARCELONA

FC Barcelona: Kiungo Iniesta kuikacha klabu yake mwisho wa msimu

Kiungo mkongwe wa klabu ya FC Barcelona ya nchini Hispania Andres Iniesta ametangaza kuwa ataiacha klabu hiyo mwishoni mwa msimu wa ligi kuu.

Kiungo wa FC Barcelona Andres Iniesta akitokwa na machozi wakati akitangaza kuachana na klabu hiyo mwishoni mwa msimu. Ijumaa, April 27, 2018.
Kiungo wa FC Barcelona Andres Iniesta akitokwa na machozi wakati akitangaza kuachana na klabu hiyo mwishoni mwa msimu. Ijumaa, April 27, 2018. REUTERS/Albert Gea
Matangazo ya kibiashara

Kiungo huyu wa timu ya taifa ya Uhispania ameichezea klabu yake mara 669 katika misimu 16, akishinda mataji 31 akiwa na Barcelona na mataji matatu makubwa akiwa na timu yake ya taifa.

Iniesta ambaye amekuwa akitajwa kuwa huenda akaenda kujiunga na klabu moja inayocheza ligi kuu ya Uchina Super League, hajasema ni wapi atacheza soka msimu ujao.

“Nilisema sitacheza kamwe dhidi ya Barcelona na hivyo haitakuwa Ulaya,” alisema kiungo huyo.

“Tutajua mwishoni mwa msimu bado kuna mambo mengi ya kufikiria.”

Iniesta alishinda taji la kombe la dunia mwaka 2010 akiwa na timu yake ya taifa ya Uhispania, akashinda michuano ya Ulaya mwaka 2008 na 2012 pamoja na mataji manne ya klabu bingwa barani Ulaya UEFA na mataji nane ya ligi kuu ya Uhispania na hivi karibuni anatarajia kutwaa taji lake la 9.

“Ni siku ngumu sana kwangu kuwa hapa na kusema kwaherim nimetumia muda wa maisha yangu yote hapa,” alisema iniesta huku akitokwa na machozi akiwa ameambatana na wachezaji wenzake pamoja na familia.

Iniesta amekuwa kiungo muhimu kwenye klabu yake ya Barcelona msimu huu, akishuhudia timu yake ikipata ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Sevilla kwenye michuano ya kombe la Copa de Rey.

Timu yake imebakiza mechi tano kumaliza msimu na watafanikiwa kutwaa taji la msimu huu ikiwa wataepuka kipigo dhidi ya klabu ya Deportivo la Coruna siku ya Jumapili.

Katika maisha yake ya soka Iniesta amecheza kwenye klabu ya FC Barcelona pekee na anakuwa mchezaji wa pili kucheza mechi nyingi zaidi kwenye klabu hiyo nyuma ya Xavi, kiungo mwenzake aliyedumu kwa muongo mmoja kabla ya kutangaza kuiacha klabu hiyo mwaka 2015 na kujiunga na timu ya Al Sadd ya Qatar.