CAF-CECAFA-SOKA

Ukanda wa CECAFA watafuta mwakilishi mashindano ya Afrika kwa vijana mwaka 2019

Rwanda ikicheza na Burundi katika mechi ya kufuzu fainali ya Afrika kwa vijana wasiozidi miaka 17
Rwanda ikicheza na Burundi katika mechi ya kufuzu fainali ya Afrika kwa vijana wasiozidi miaka 17 www.cafonline.com

Timu ya taifa ya soka ya Rwanda inaongoza kundi la A, katika mashindano ya kufuzu kuwakilisha ukanda wa Afrika Mashariki na Kati CECAFA, katika mashindano ya bara Afrika kwa wachezaji wasiozidi miaka 17, itakayofanyika mwaka 2019 nchini Tanzania.

Matangazo ya kibiashara

Mashindano hayo ya kufuzu yanaendelea nchini Tanzania katika jiji la Dar es salaam na yanayakutanisha mataifa tisa.

Rwanda inaongoza kundi la A, kwa alama sita baada ya kushinda mechi mbili, dhidi ya Sudan mabao 3-1 na Burundi mabao 4-3.

Tanzania ambao watakuwa wenyeji, wamepata ushindi mara moja hadi sasa hivi dhidi ya Burundi kwa mabao 2-1.

Kundi hili lina Sudan ambayo haijapata ushindi katika mchuano wowote. Somalia ilijiondoa katika mashindani haya.

Mechi za kundi hili zinaendelea wiki hii, siku ya Alhamisi Sudan itacheza na Tanzania, huku Burundi na Sudan ikimenyana siku ya Jumamosi. Mechi za kundi hili zinachezwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Ethiopia na Kenya nazo zinapambana katika kundi B, ambalo pia lina Sudan Kusini, Uganda na Djibouti.

Kundi hili linaloongozwa na Ethiopia kwa alama sita, baada ya kushinda mechi mbili dhidi ya Uganda bao 1-0 na Djibouti mabao 4-0.

Kenya ina alama tatu baada ya kushinda mechi yao ya kwanza dhidi ya Sudan Kusini kwa kupata ushindi wa mabao 4-0.

Siku ya Ijumaa, kutakuwa na mechi mbili katika uwanja wa Chamazi nje, kidogo ya jiji la Dar es salaam kati ya Sudan Kuisni na Uganda lakini pia kati ya Djibouti na Kenya.

Mshindi wa kwanza na wa pili katika kila kundi atafuzu katika hatua ya nusu fainali, huku fainali ikichezwa tarehe 26 na mshindi atafuzu katika fainali hizo za bara Afrika.